NI ujambazi wa kutisha. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kuibuka na wizi unaofanywa na majambazi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hiyo inatokana na majambazi hao kuibuka na mbinu mpya kila kukicha katika matukio mbalimbali ambayo sasa yamekuwa yakishika kasi.
Mbali na mbinu ya kutumia pikipiki, majambazi hayo pia huvamia vibanda vya kutoa huduma za fedha, kuiba magari na hata wakati mwingine kuua.
Katika hali iliyovuta hisia za watu wengi, juzi usiku majambazi yalifunga mtaa kwa saa mbili na kupora fedha kwa watoa huduma ya fedha kwa njia ya simu katika eneo la Tabata jijini Dar es Salaam.
Mbali na maduka, watu wengine waliokuwa nje nao pia waliporwa simu na fedha. Hata hivyo thamani ya fedha na vitu vilivyoporwa havikujulikana mara moja.
Tukio hilo lililoshtua wakazi wengi wa mitaa ya Kimanga na Kisukuru wilayani Ilala, Dar es Salaam, ni la pili kutokea ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.
Awali mwezi uliopita, majambazi wenye silaha walimuua kwa risasi askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na baadaye kumpora fedha Sh milioni tano, nje ya geti la nyumbani kwake Mtaa wa Kimanga, saa tano asubuhi.
Tukio la juzi lilitokea katika moja ya maduka yaliyoko pembezoni mwa kituo cha daladala cha Jiandae kilichopo Tabata Kimanga, ambako majambazi wanaokadiriwa kuwa zaidi ya wanne yaliingia dukani na kuwaamuru wafanyakazi kutoa fedha zote za mauzo ya siku, huku wakiwatishia kwa mapanga na bastola.
Mmoja wa wafanyakazi wa kike katika maduka hayo alipoteza fahamu baada ya tukio hilo na alikimbizwa hospitali kwa matibabu.
Licha ya idadi kubwa ya watu katika eneo hilo lenye biashara mbalimbali wakati wa jioni, majambazi hao hawakujali, walifanya uporaji huo na baadaye kutokomea kwa kutumia pikipiki aina ya Boxer.
Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia MTANZANIA jana kuwa kwa muda wa dakika tano hakuna gari iliyoruhusiwa kwenda au kutoka Kimanga.
“Majambazi waliwaamuru wenye magari kutokukatiza eneo hilo, huku waenda kwa miguu wakiamriwa kuondoka haraka.
“Katika hali ya kawaida ni vigumu kuamini kama majambazi wanaweza kuvamia na kupora vitu katika maduka matatu kwa mpigo halafu wakatoweka bila kukamatwa,” alisema shuhuda huyo aliyekataa kutajwa jina.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Manase Mjema, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema majambazi hao yalikuwa yamejiandaa na yalitumia silaha kubwa.
“Awali kabla ya kufyatua risasi yaliwaamuru wafanyakazi wa maduka yanayofanya biashara kupitia miamala ya simu kutoa fedha zote za mauzo, vijana walikuwa ngangari kidogo, hivyo majambazi waliamua kupiga risasi tatu hewani ndipo waliamua kutoa fedha walizokuwa nazo,” alisema.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikiri kuwapo kwa ulinzi hafifu katika mtaa wake, huku pia akishauri Jeshi la Polisi kuimarisha doria mitaani kwa kuongeza askari wasiokuwa na sare ili wasitambulike kwa urahisi.
“Nikiri kwamba ulinzi wetu wa mtaa wakati wa usiku bado ni mdogo, tunaomba polisi nao waangalie mbinu mbadala za kukabiliana na uhalifu, na hasa ujambazi huu wa kutumia silaha za moto. Eneo la Tabata hivi sasa limekumbwa na matukio mengi ya ujambazi, kwa hiyo lazima mbinu nazo zibadilike,” alisema Mjema ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kimanga (Chadema).
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, alikiri kupokea taarifa za ujambazi na tayari askari wake wameanza uchunguzi ili kuwabaini wahalifu hao.
“Nitoe ombi na nisisitize wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kutokomeza vitendo vyote vya uhalifu. Viongozi wote wa mitaa watupatie taarifa za watu wanaowatilia shaka, nasi tutazifanyia kazi,” alisema Kamanda Mkondya.
Katika siku za hivi karibu kumeibuka matukio ya ujambazi katika maeneo mbalimbali nchini huku wakiibua mbinu mpya za kufanikisha wizi huo.
Kutokana na hali hiyo majambazi hao wamekuwa wakitumia pikipiki kwa ajili ya kutekeleza uvamizi kwenye matukio hayo na hata wakati mwingine kuua watu na kujeruhi.
Katika mfululizo wa matukio ya ujambazi jijini Dar es Salaam, Agosti 23, mwaka huu, askari wanne wa Jeshi la Polisi waliuawa baada ya majambazi kuvamia Tawi la Benki ya CRDB lililopo Mbande, wilayani Temeke.
Majambazi hao wanaokadiriwa kufikia 14, wakati askari hao wakibadilishana lindo, waliibuka ghafla na kuanza kurusha risasi na askari mmoja aliyekuwa lindo alifanikiwa kukimbia.
Kutokana na foleni katika barabara nyingi za Dar es Salaam pamoja na miundombinu ya makazi yasiyokuwa rasmi, matukio mengi ya ujambazi yanayoripotiwa ni ya kutumia pikipiki, hivyo kuwapa wakati mgumu polisi ambao mara nyingi wanatumia magari ya doria.
Mapema mwaka huu Rais Dk. John Magufuli aliliagiza Jeshi la Polisi kutumia mbinu za kisasa katika kukabiliana na uhalifu na kuifanya nchi kuwa sehemu salama nyakati zote.
Dk Magufuli alionesha kushangazwa na askari wa Jeshi la Polisi kunyang’anywa silaha yake na majambazi na wakati mwingine kuuliwa na majambazi, akihoji uwezo wa majambazi kiasi cha kuwatesa polisi kiasi hicho.
Rais alikuwa akizindua Mpango wa kuboresha usalama wa jamii na mali zao, ambao una dhamira ya kupunguza uhalifu ambapo ameliagiza jeshi hilo kuwahi kushughulikia majambazi kabla ya wenyewe kushughulikiwa na majambazi hayo.
Pamoja na hali hiyo Jeshi la Polisi lilitangaza mikakati mbalimbali ikiwamo ukaguzi maalumu wa bodaboda na kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu ili kufuatilia matukio mbalimbali.
Majambazi hao ambao kwa muda sasa wamekuwa wakiibuka na mbinu mpya ikiwamo ya kutumia bodaboda kuvamia benki na wanaotoka benki na kuwapora fedha.
Licha ya polisi kuweka ulinzi maalumu na waendesha bodaboda watakaoonekana kupakia kitu chochote na kukiweka mbele (katika tenki la mafuta) au kiti cha nyuma, ikiwemo kusimamishwa na kupekuliwa lakini bado mbinu hiyo imekuwa ikifeli na watu wakijikuta wakidhurika.
Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wananchi kuvamiwa na kuporwa fedha, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuzichukua benki huku wafanyakazi wa benki wakidaiwa kuhusika kutoa taarifa za wateja.
Mara zote majambazi hutumia bodaboda kufanikisha uhalifu huo, huku wakiwa na silaha ambazo huzitumia kutishia, kujeruhi na wakati mwingine kuua.
Na ARODIA PETER-MTANZANIA DAR ES SALAAM
Social Plugin