Upepo mkali ukiambatana na mvua umeezua nyumba 44 katika
Kijiji cha Kiemba Kata ya Ifulifu, Wilaya ya Musoma mkoani Mara.
Kati ya
nyumba hizo, tano ziliathirika vibaya kiasi cha kusababisha wamiliki
wake kulala nje. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
alikagua baadhi ya nyumba zilizoathirika ili kuona athari za uharibifu
huo.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Vicent Naano na viongozi wa
halmashauri, walitembelea eneo hilo baada ya kupata taarifa za athari za
kuezuliwa paa na kuagiza tathmini ifanyike ili Serikali iweze kutoa
msaada kwa wananchi hao.
Profesa Muhongo aliwaambia waathirika hao
kuwa Serikali ya Rais John Magufuli ipo pamoja nao na ametumwa kuwapa
pole kutoka kwa viongozi wa juu wa Serikali.
“Ndugu wananchi, nimetumwa na Rais wetu Dk John Magufuli niwape pole sana kwa kukutwa na
kadhia hii ya kuezuliwa na upepo kwa paa za nyumba zenu. Makamu wa Rais
na Waziri Mkuu wanawapa pole pia na wanawatakia heri wale wote
walioathirika,” alisema.
Profesa Muhongo aliwaelekeza viongozi wa
kijiji hicho wahakikishe wanafanya tathmini ya kweli kwa kupita kila
nyumba iliyoathirika na yoyote atakayegundulika amedanganya ili Serikali
imlipe, zoezi zima litaahirishwa na kurudiwa upya, pia wahusika
watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aliwaahidi wananchi hao kuanza kupewa
misaada baada ya kikao cha halmashauri kupitia taarifa ya tathmini
kesho, na kuwaelekeza viongozi kufanya kazi hiyo kwa haraka.
Profesa
Muhongo alikuwa mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya kukagua umeme na
kushiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere iliyofanyika nyumbani kwake Butiama juzi.
Social Plugin