Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewakamata raia wawili wa China kwa makosa ya utekaji nyara mfanyakazi wa kasino ya Le Grande iliyopo maeneo ya Upanga, ambaye pia ni mchina aliyefahamika kwa jina la Liu Hong (48).
Kamishna wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro leo amewaambia waandishi wa habari kuwa, wachina hao walimteka Hong na kumfanyia vitendo vya ukatili ambapo walitoa masharti ya kupatiwa dola za kimarekani 19,000 ili wamuache huru.
Kamanda Sirro amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Wang Young Jing (37) na Chen Chung Bao (35).Amesema watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi katika chumba walichomficha Hong walikuta bomba la sindano, kamba za plastiki ambavyo vinasadikika kutumika kumjeruhi raia huyo wa china.
Amesema baada ya askari polisi kufanikiwa kumuokoa Hong walimpeleka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
Aidha, Kamanda Sirro ametoa taadhari kwa wakazi wa Dar es Salaam kuwa makini na raia wa kigeni waishio nchini kwa kuwa baadhi yao hushughulika na uhalifu ikiwemo utekaji nyara.
Amewataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini kuwa kuna raia wa kigeni wanaonyanyasa wazawa na kufanya vitendo vya kihalifu.