Baada ya wakazi wa Kijiji cha Iringa Mvumi katika Wilaya ya
Chamwino mkoani Dodoma kuwaua watafiti wa Kituo cha Udongo na Maendeleo
cha Selian Arusha, wakazi wa kijiji hicho wamehama makazi yao wakihofia
kukamatwa na Jeshi la Polisi.
Waandishi wa habari waliofika kijijini hapo jana na walishuhudia hali ya utulivu kijijini hapo tofauti na ilivyozoeleka.
Pamoja
na wananchi hao kukimbia makazi yao, taarifa zinasema viongozi wote wa
Serikali ya Kijiji hicho wamekamatwa na polisi wakiwamo Mwenyekiti wa
Serikali ya Kijiji, Albert Chimanga na Diwani wa Kata ya Iringa Mvumi,
Robert Chikole.
Mmoja
wa wakazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Michael Kagisi,
alisema kitendo cha wananchi kukimbia kijiji hicho kimesababisha
shughuli nyingi za jamii kusimama na maduka kufungwa.
Kwa
mujibu wa Kagisi, hata wananchi waliobaki kijijini hapo wakisema
hawakushiriki mauaji hayo, ikifika jioni wanakwenda porini kulala.
“Sehemu
kubwa ya watu wameyakimbia makazi yao kwa sababu wanaogopa kukamatwa na
polisi, yaani hata shule hazina wanafunzi kwa sababu wengi wamekimbia
na wazazi wao.
“Yaani
waliouawa waliuawa kwa makosa kwa sababu kabla ya kuwapiga,
walijitetea na kujitambulisha, lakini wananchi hawakutaka
kuwasikiliza… baada ya kuwaua, waliwawekea majani na kuwachoma moto
ili wafe haraka,” alisema Kagisi.
Akifafanua,
mwananchi huyo alisema siku ya tukio ulikuwapo mkutano kijijini hapo na
mwenyekiti wa kijiji alipata taarifa kwamba katika eneo la kutengeneza
chumvi, kuna gari ambalo walilitilia shaka kwamba huenda ni majambazi.
“Siku hiyo tulikuwa kwenye mkutano na baadaye tulimuona mwenyekiti akiwaita baadhi ya vijana na kuwaagiza waende eneo la tukio.
“Wale vijana walikwenda huko walipiga simu kijijini kuwaeleza wananchi, kwamba kuna gari la watu ambao hawaeleweki.
“Taarifa hizo ziliposambaa, wananchi walihamasishana na kuelekea eneo la tukio.
“Walipofika
tu, walianza kuwapiga, lakini wale watafiti walijieleza kwamba wao siyo
majambazi, huku wakiwaomba wananchi wawapeleke katika ofisi zao za
kijiji, lakini wananchi walikataa na kuendelea kuwapiga hadi
walipowaua,” alisema.
Naye
Mchungaji wa Kanisa la Biblia kijijini hapo, Donald Nyambuya, alisema
kwa sasa maisha kijijini hapo ni ya shida kwa sababu huduma nyingi za
jamii zimefungwa baada ya watu kukimbia makazi yao.
Mwinjilisti
wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jacob Foda, alisema kitendo
cha watu kukimbia makazi yao kimeathiri huduma ya roho kwa kuwa huwa
na kawaida kuwatembelea waumini wake.
Wakati
huohuo, simanzi na majonzi, jana, vilitawala wakati wa kuaga miili ya
Watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Udongo na Maendeleo cha Selian mjini
hapa.
Watafiti
hao waliuawa juzi na wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani
Chamwino, Mkoa wa Dodoma kwa kukatwakatwa mapanga na kuchomwa moto.
Miili
hiyo iliwasili mjini hapa jana asubuhi kwa gari ikitokea Dodoma na
kuingizwa kwenye eneo la wazi la kituo hicho kilichopo pembeni mwa
Uwanja mdogo wa Ndege wa Arusha kwa ajili ya wafanyakazi kutoa heshima
za mwisho.
Shughuli
ya kuaga miili hiyo ilifanyika asubuhi kwa wafanyakazi, jamaa na
marafiki kutoa heshima za mwisho bila majeneza kufunguliwa kwa kuwa
imeharibika.
Baadaye ilipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa ajili ya kufanyiwa maandalizi ya kusafirishwa.
Waliouawa
katika tukio hilo walitambuliwa kuwa ni Jaffari Mafuru aliyesafirishwa
jana kwenda Mara kwa mazishi, Theresia Ngume, aliyetarajiwa kuzikwa
jana mjini Arusha na dereva wa gari walilokuwamo, STJ 9570 aina ya
Toyota Hilux, mali ya Kituo cha Utafiti cha Selian, Nikas Magazine,
aliyesafirishwa kwenda Ifakara, Morogoro kwa mazishi.
Watafiti hao waliuawa wakiwa katika kazi ya mradi unaoandaa taarifa za hali ya udogo kwa nchi nzima.
Akizungumza
baada ya kutoa heshima za mwisho, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Januari
Mafuru ambaye ni baba mzazi wa marehemu Jaffari, alisema tukio hilo
limemuumiza sana.
Alisema
kituo hicho kimekuwa kikiendesha mradi huo kwa lengo la kuwasilisha
taarifa hizo kwa wakulima wadogo na wataalamu wa kilimo ziweze
kuwasaidia wananchi katika kilimo na hatimaye kuongeza mazao.
“Mradi
huu umemaliza utafiti katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya
Kilimanjaro, Arusha na Manyara. Baada ya hapo kazi nyingine ilikuwa
imeanza Kanda ya Kati Dodoma na Singida.
“Wiki
iliyopita, tuliandaa watafiti wanane na magari yao manne kwa ajili ya
kwenda mkoani Dodoma kukusanya udongo kwa ajili ya kuuleta hapa kwenye
maabara za Seliani kufanyiwa utafiti kisha kutoa matokeo yatakayowarudia
wakulima,” alisema Mafuru.
Akizungumzia
kuwasili kwa watafiti hao katika Kijiji cha Iringa Mvumi, wilayani
Chamwino yalikotokea mauaji hayo, Mafuru alisema timu zote zilikuwa na
barua za utambulisho pamoja na vifaa vya kazi.
“Timu
iliyokuwa Chamwino katika Kijiji cha Iringa Mvumi, iliwakuta wanawake
wakiendelea na shughuli za kukusanya chumvi na watafiti waliwasilimia
na kujitambulisha wametokea wapi.
“Taarifa tulizonazo ni kwamba, baada ya kusalimia, watafiti waliacha gari pembeni na kutembelea maeneo kuchagua udogo.
“Huku
nyuma kundi la wale wanawake lilitoa taarifa kwa viongozi wao kuwa
wamevamiwa na wanyonya damu, ndipo walipotokea watu wakiwa na mashoka na
mapanga na kuwashambulia kabla ya kuwachoma moto,” alisema.
Mtafiti
Mwandamizi wa Kituo cha Selian, Dk. Lameck Makoye, alilaani mauaji hayo
na kusema hajawahi kuona wala kusikia watafiti wakivamiwa
wanapokuwa vijijini.
“Naamini
Serikali imeona, binafsi sijawahi kuona tukio la aina hii kwa sababu
watafiti wale walikuwa na vielelezo vyote vinavyowatambulisha.
“Hata
mradi waliokwenda kufanya ulikuwa ni kwa faida ya wananchi wa Kijiji
cha Iringa Mvumi kwa vile umelenga maeneo ya nchi nzima.
“Sisi
Kituo cha Utafiti cha Selian ndiyo tunaoleta maendeleo ya mkulima kwa
nchi nzima kwa kufanya utafiti wa udongo unaomwezesha mkulima alime vipi
na atumie mbolea kwa kiwango gani na ya aina gani,” alisema Dk. Makoye.
Mume
wa marehemu Theresia, Jonas Mjema, akizungumza kwa huzuni kuhusu
kuondokewa na mkewe, alisema kabla ya tukio la mkewe kuchomwa moto,
alizungumza naye asubuhi kujua anaendeleaje.
“Niliwasiliana naye asubuhi Jumamosi tukatakiana kazi njema, ilipofika jioni nilimtafuta lakini simu yake haikupatikana.
“Nilijipa matumaini labda mawasiliano hayakuwa mazuri kwa vile shughuli zao ni za porini.
“Ilipofika Jumapili, nilipigiwa simu na shemeji yangu akinipa taarifa za tukio la kuchomwa moto mke wangu,” alisema Mjema aliyeachwa na watoto wawili.
Social Plugin