Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU SITA WANASWA NA POLISI WAKIWA NA SILAHA ZA MOTO NYUMBANI KWA MGANGA WA KIENYEJI

 
POLISI mkoani Mwanza imewakamata watu sita wakiwa na silaha mbili zilizotengenezwa kienyeji, walizokuwa wakizitumia kwenye matukio ya unyang’anyi na uporaji wa mali, zikiwa zimehifadhiwa kwa mganga wa kienyeji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa watu hao wamekamatwa Oktoba 18, mwaka huu saa saba mchana, baada ya polisi wakiwa kwenye doria Buswelu, kata ya Buswelu, Manispaa ya Ilemela, waliwakamata watu hao baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wa wahalifu hao.

Katika hatua za awali, polisi walimkamata Jeremia Mkumbo (25) mkazi wa Malega mkoani Singida.

“Alipohojiwa alikiri kuhusika kwenye matukio ya uhalifu na kuwataja watu wengine waliokuwa wakishirikiana.Alisema silaha ambazo hutumia kwenye uhalifu waliziacha kwa mganga wa kienyeji aitwaye Leonard Litta mkazi wa mtaa wa Kagida- Buswelu”, alifafanua Kamanda Msangi.

Alisema polisi walikwenda nyumbani kwa mganga huyo wa kienyeji, Leonard Litta (39) na baada ya kufanya upekuzi nyumbani hapo, walikamata risasi 22 zinazotumiwa na bunduki aina ya short gun.

Alisema baada ya kuhojiwa na polisi, watuhumiwa hao waliwataja watu wengine wanne waliokuwa wakishirikiana katika kufanya uhalifu ambao nao wamekamatwa.

Aliwataja watu waliokamatwa kuwa ni Kamugisha Jovin (40) mlinzi na mkazi wa Iloganzala, Juma Yusuph (35) mkazi wa Bwani –Kinondoni, Samwel Peter (36) mkazi wa Buswelu na Shaban Hussein (26) fundi viatu na mkazi wa Nyasaka Msumbiji katika Manispaa ya Ilemela.

“Watuhumiwa wote walipofanyiwa mahojiano walikiri kuwa walizitumia silaha hizi katika unyang’anyi wa mali na uporaji katika maeneo ya jiji na mkoa wetu wa Mwanza”, alieleza na kuongeza kuwa Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na mengine waliyoyafanya na pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

Katika tukio lingine, Kamanda Msangi alisema Polisi imewakamata wakazi wawili wa Dar es Salaam waliokutwa na gari la wizi.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 18, mwaka huu saa nane mchana eneo la Ilemela Manispaa ya Ilemela, wakiwa kwenye harakati za kuuza gari lenye namba za usajili T.778 AZV aina ya Toyota Land Cruiser, walilokuwa wameliiba kwa mfanyabiashara wa Kiasia, Ilala jijini Dar es Salaam.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Rahim Feka (28) mkazi wa Ilala na Ally Kawale (32) mkazi wa Jet Lumo- Airport.

Aliongeza kuwa watuhumiwa hao, walikamatwa baada ya Polisi kupokea taarifa za kuibwa kwa gari hilo kutoka jijini Dar es Salaam.

“Baada ya kupata taarifa kutoka Dar es Salaam, tulihisi kuna uwezekano wa mtandao huu wa wizi wa magari kuwepo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa na baada ya kufanya uchunguzi tulifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao,” alisema Kamanda Msangi na kuongeza kuwa watuhumiwa wote wako chini ya ulinzi wa Polisi kwa mahojiano zaidi.

Alisema Polisi mkoani Mwanza inawasiliana na wenzao wa Dar es Salaam, kufanya taratibu za kuwasafirisha watuhumiwa hao.
Imeandikwa na Nashon Kennedy-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com