Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpa maelekezo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mkoa wa Lindi (LUWASA), Adam Alexanda muda mfupi kabla ya kumsimamisha kazi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Lindi (LUWASA), Mhandisi Adam Alexander kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi pamoja na kushindwa kusimamia ujenzi wa kituo cha kuzalisha maji katika Manispaa ya Lindi.
Waziri Mkuu amemkabidhi mhandisi huyo kwa Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi, Stephen Chami na kumuelekeza afanye uchunguzi zaidi juu ya suala hilo.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea mradi wa maji wa Ng’apa, ambapo aliagiza nafasi hiyo ikaimiwe na Mkurugenzi Msaidizi wa mamlaka hiyo, Mhandisi Idrisa Sengulo.
“Kamanda wa Takukuru fanya mapitio ya kina ya mshahara wake. Yeye anasema analipwa mimi najua analipwa na Luwasa. Angalia kazi aliyokwenda kuifanya Dar es Salaam kama inalingana na siku alizokaa,” alisisitiza Waziri Mkuu katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi yake jana.
Mhandisi hiyo anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za ofisi pamoja na kupokea mshahara bila ya kulipa Kodi ya Mapato ya Mshahara (PAYE), kujilipa kiwango kikubwa cha posho pamoja na kusafiri kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu alisema serikali haiwezi kuvumilia kuona wananchi wanapata shida huku watendaji waliopewa dhamana ya kuwatumikia, hawaonekani kwenye vituo vyao vya kazi.
“Huyu nimemuita mimi aje huku, hadi jana alikuwa Dar es Salaam,” alieleza Majaliwa.
Alipoulizwa sababu za kutokuwepo ofisini kwake kwa muda mrefu, Mkurugenzi huyo alisema kwamba alikuwa Dar es Salaam akiandika maombi ya fedha kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo.
“Unatumia siku ngapi kuandika proposal, msomi unatumia mwezi mzima kuandika proposal na unakaa Dar es Salaam hata Katibu Mkuu wako hajui na huko unajilipa posho tu! Tena baada ya kulipwa shilingi 120,000 kwa siku wewe unajilipa shilingi 150,000. Hatuwezi kuvumilia hali hii,” alisema.
Waziri Mkuu alimaliza ziara yake yansiku tatu mkoani Lindi na alirejea jijini Dar es Salaam.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin