WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA ATUA RASMI DODOMA,ASEMA SIYO TUKIO LA MZAHA,HAWAFANYI MAJARIBIO


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary (nyuma) wakiwapungia wananchi baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma jana, kuanza makazi mapya ya kiutawala.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



TANZANIA jana iliandika historia mpya baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasili uwanja wa ndege wa Dodoma na kudhihirisha wazi kuwa sasa Dodoma ni makao makuu ya nchi na serikali yote itahamia Dodoma.

Alipokewa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenister Mhagama na mamia ya wakazi wa Dodoma.

Ndege iliyombeba Waziri Mkuu iliwasili uwanja wa ndege saa 10.06 alasiri, ambapo alishuka ndani ya ndege akiwa ameongozana na mkewe, Mary, kisha kuwapungia wananchi.

Nje ya uwanja wa ndege, wananchi walijipanga barabarani wakiwa wamesimama na mabango, kama ishara ya kumkaribisha mkoani hapa kiongozi huyo wa juu, ambaye aliahidi Watanzania kuwa angehamia rasmi Dodoma mwezi Septemba.

Miongoni mwa mabango hayo yalisomeka ‘Magufuli Oyee’, ‘Ndege Tumeziona’, ‘Majaliwa Tumemuona’, ‘Tunakukubali’.Mabango mengine yalisomeka ‘Magufuli Tumemkubali, ‘Endelea kutumbua majipu’.

Kutoka Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwenda makazi ya Waziri Mkuu yaliyopo eneo la Mlimwa, wananchi wenye baiskeli, pikipiki na wengineo walijipanga kandokando ya barabara huku wakipunga matawi ya miti kuonesha furaha yao ya serikali kuanza kuhamia Dodoma.

Akizungumza nyumbani kwake Mlimwa mjini hapa, Majaliwa alisema waliosema serikali haiwezi kuhamia Dodoma wameumbuka, kwani serikali imehamia rasmi na wanaohitaji huduma ya Waziri Mkuu wataifuata Dodoma.

“Tukio hili si la mzaha, ni la kweli na nimeshafika Dodoma,” alisema na kuwataka mawaziri, naibu mawaziri na makatibu wakuu wajipange kwa safari ya Dodoma. Pia, alisema hata Rais amesema asiyehamia Dodoma, atakuwa amejiondoa kazini.

Alisema kitendo cha serikali kuhamia Dodoma, si tukio la kawaida. Alisema amefarijika kuona barabara nzima, zilijaa watu wenye furaha kwa ajili ya kumkaribisha Dodoma.

“Mchana kabla ya kwenda kupanda ndege, nilienda kumuaga Rais na Makamu wa Rais, nikaulizwa naondoka kwa usafiri gani nikasema kwa ndege, Rais na Makamu wake wanawasalimia; na wamesema tukio hili si siasa wala majaribio, kama kuna mtu alifikiria jambo hili halitekelezeki, si kwa awamu hii,” alisema.

Alisema kuanzia leo serikali iko Dodoma; na yeyote anayeitaka huduma ya Waziri Mkuu, ataipata Dodoma. Alisema Dodoma ina uwezo wa kupokea watumishi wote wa serikali na wakaweza kufanya kazi zao kikamilifu.

Via>>Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post