Majeneza ya watalii hao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelaani kitendo cha wanakijiji kuwaua watumishi wa Serikali waliokuwa wakifanya utafiti wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo (Jumanne, Oktoba 3, 2016) wakati akizungumza na waandishi wa habari wa mkoa wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kukutana na makundi mbalimbali.
Mauaji ya watafiti hao, Teddy Nguma, Jafari Mafuru na dereva wao Bw. Nicas Magazine yalitokea Oktoba Mosi, 2016 baada ya kushambuliwa na wakazi wa kijiji cha Makang’wa wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Amesema Serikali imesikitishwa na mauaji ya watu watatu wakiwemo watafiti wawili kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Seliani (SARI) kilichopo mkoani Arusha ambao walikuwa kazini kuchunguza sampuli za udongo ili kubaini kama matetemeko yataendelea kutokea.
“Kutokana na tetemeko lilitokea mkoani Kagera, Serikali iliamua kushirikisha watalaamu mbalimbali kufanya uchunguzi kuona kama tetemeko hilo ni endelevu au la katika maeneo mengine. Kitendo cha watu kujichukulia hatua mkononi na kukatisha uhai wa watumishi ambao walikuwa kazini hakikubaliki,” amesema
Amesema watalaamu hao walifika katika Wilaya ya Chamwino na kufanya kazi kwa siku tano na siku ya sita ndipo walipoenda eneo la kijiji cha Iringa Mvumi kuendelea na kazi ambapo waliuawa wakiwa kazini.
“Serikali kupitia kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa inaendelea na uchunguzi wa kuwabaini watu waliofanya kitendo hicho’’ amesema. Hata hivyo, Waziri Mkuu amewatoa wasiwasi watumishi wanaohamia Dodoma kuwa Dodoma ni salama na kila anayekuja yupo salama. “Dodoma ipo salama na tunatarajia kila anayehamia hapa atakuwa salama na hata wakazi wa hapa wataendelea kuwa salama,’’ amesema.
Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri Mkuu amesema hali hiyo inajitokeza hivi sasa baada ya wananchi wengi kutambua thamani ya ardhi.
Amesema miaka ya nyuma watu wachache walitambua thamani ardhi hivyo kuchukua maeneo makubwa na kuyamiliki. Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa migogoro hiyo inamalizika kwa kuweka kuweka msisitizo kuwe mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwa ni pamoja na kupima ardhi yote na kutoa hati kwa wananchi.
“Tunataka ardhi yote ipimwe na kila mtu anayepewa ardhi apewe hati ya kumiliki na si vinginevyo’’ amesema. Wakati huohuo, Waziri Mkuu aliwaasa waandishi wa habari wawe makini na kazi yao na wajiepushe na upotoshaji kwenye taarifa wanazozitoa kwa wananchi. Amesema vyombo vya habari ni kiungo muhimu baina ya Serikali na wananchi, hivyo aliwataka viongozi wote wa umma washirikiane na vyombo vya habari kwa kutoa habari za utekelezaji wa kazi za Serikali.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea msaada wa sh. milioni 11.42 kutoka kwa taasisi na wadau mbalimbali mkoani Dodoma zikiwa ni kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, 2016 na kusababisha vifo vya watu 17.
Michango aliyopokea leo imetolewa na Mzee Thakar Singh na familia yake sh. milioni 5; NSSF Dodoma (sh. milioni 1.2); Shirika la Bima ya Taifa tawi la Dodoma (sh. milioni moja); Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (sh. milioni moja) na Ofisi Rais TAMISEMI (sh. milioni 2). Wengine ni TRA-Dodoma (sh. milioni moja); Dodoma FM (sh. 200,000) na Mwalimu Mstaafu, Mama Amina Mafuru aliyetoa sh. 20,000/-.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA. JUMANNE, OKTOBA 04, 2016
Social Plugin