Katika uamuzi mkubwa uliotarajiwa na wengi,Eric Aniva alipatikana na hatia ya ''kutekeleza mila zenye madhara'' chini ya sheria za kijinsia za taifa hilo baada ya uchunguzi wa BBC kubaini vile alivyolipwa ili kuwafanyia sherehe za kutakasa wasichana wadogo pamoja na wanawake wajane.
Eric Aniva ni mwanamume wa kwanza kufungwa jela kuwa 'fisi' neno linalotumika kwa mwanamume anayelipwa ili kushiriki ngono na wanawake pamoja na wasichana ikiwa ni miongoni mwa tamaduni za kutakasa.
Katika mahojiano na BBC ,alikiri kufanya mapenzi na wanawake 104 na wasichana bila kuwalezea kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vya HIV.
Ijapokuwa hakuna msichana aliyejitokeza, kulalamika, alipatikana na hatia ya kutekeleza mila zenye madhara baada ya wanawake wawili kutoa ushahidi wao.
Wote wawili ni wajane ambao wanasema walilazimishwa kufanya mapenzi na mtu huyo ili kutakasa roho za waume zao baada ya vifo vyao.
Kesi hiyo imezua maoni tofauti nchini Malawi huku baadhi yao wakidai kwamba sheria kali za kijinsia zinaingilia utamaduni na kwamba bw Aniva anasulubiwa .
Wakati huohuo mashirika ya haki za kibinaadamu yanaamini kwamba kesi hiyo ni ushindi katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kingono.
Chanzo-BBC
Social Plugin