SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limewashtaki kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baadhi ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri na manispaa, wanaowaweka ndani na kuwashusha vyeo watumishi wa umma bila sababu za msingi.
Malalamiko hayo yalitolewa jana mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya, alipokuwa akisoma risala katika mkutano mkuu wa sita wa shirikisho hilo mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa.
Pamoja na Majaliwa, walikuwapo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenister Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angelah Kairuki.
Katika maelezo yake, Mgaya alilalamikia tabia ya viongozi hao na kusema inakatisha tamaa watumishi wa umma kwa kuwa wanafanya kazi kwa hofu.
Kwa mujibu wa Mgaya, utaratibu huo hawakubaliani nao kwa kuwa umekuwa ukifanywa bila ya kufuata kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
“Sisi kama viongozi wa vyama vya wafanyakazi, hatukubali jinsi viongozi hao pamoja na wanasiasa wengine, wanavyowafukuza kazi watumishi kwa kutaka mambo yao yaende vizuri.
“Tungependa kuona sheria zinafuatwa pale ambapo masuala ya nidhamu ya mfanyakazi yanahusika ili kuondoa maonevu yasiyokuwa ya lazima, kwani hata waswahili husema mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni,’’ alisema Mgaya huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.
Akijibu malalamiko hayo, Majaliwa alisema Serikali ya Rais Dk. John Magufuli itaendelea kuzingatia utawala wa sheria na kanuni za utawala bora, ili kuhakikisha haki za wafanyakazi nchini zinalindwa ipasavyo.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza viongozi wa kisiasa nchini walioko katika wizara mbalimbali, mikoani, wilayani, idara za Serikali, halmashauri na taasisi zote za Serikali, wazingatie utawala wa sheria kushughulikia masuala mbalimbali yanayohusu wajibu na haki za wafanyakazi.
“Pamoja na hayo, lazima wafanyakazi wote nchini mtekeleze majukumu yenu kwa nidhamu, muwajibike na muwe waadilifu pia.
“Ni wazi kwamba nidhamu ya kazi imeporomoka kidogo kutokana na watumishi kutotimiza wajibu wao na wengine ni wabadhilifu wa mali za umma.
“Hao Serikali haitawafumbia macho, tutaendelea kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,’’ alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Kuhusu mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, aliwaagiza waajiri wote nchini, kutoa mikataba hiyo haraka iwezekanavyo kwa wafanyakazi wao.
Pia, aliwaagiza maofisa wa kazi nchini, kuhakikisha kila mwajiri anafikiwa na watakaokutwa wakikiuka taratibu za ajira, wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Chanzo-Mtanzania
Social Plugin