RAIS John Magufuli amefichua siri ya hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya bodi hiyo kuidhinisha Sh bilioni 26 kupelekwa kuwekwa kwenye akaunti maalumu( Fixed Account) katika benki kadhaa za biashara.
Bodi hiyo ilitoa idhini ya kupelekwa fedha hizo katika benki hizo wakati kuna agizo la Rais la kupiga marufuku kwa taasisi za umma, mashirika ya umma, idara za serikali, wakala na wizara kuweka fedha zao katika benki za kibiashara.
Fedha hizo zinatakiwa zifunguliwe akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jumapili iliyopita asubuhi, Ikulu ilitangaza kwamba Dk Magufuli ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, na saa chache akateua Naibu Kamishna Mkuu mpya.
Ikulu bila kueleza sababu, ilisema kwamba Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu na kuivunja bodi nzima.
Aidha, pamoja na kuivunja bodi hiyo alimteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, kuziba nafasi iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja baada ya Dk Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa akishikilia wadhifa huo Lusekelo Mwaseba.
“Uteuzi wa Mwenyekiti mwingine wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA na Bodi ya Mamlaka hiyo utatangazwa baadaye,” ilieleza taarifa ya Ikulu iliyotolewa Jumapili asubuhi sana.
Akihutubia jana katika Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kwenye Makao Makuu ya chuo hicho, Bungo wilayani Kibaha katika mkoa wa Pwani, Dk Magufuli alisema aliitumbua bodi hiyo kutokana na kukiuka taratibu.
Alieleza kuwa kitendo chao cha kuidhinisha fedha hizo kuwekwa kwenye benki tofauti, ni tofauti na maelekezo kwani huo ndio ulikuwa mchezo unaofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali.
“Sasa sifahamu kama Chuo Kikuu Huria na nyinyi mmekuwa mkiweka fedha za maendeleo katika Fixed Deposit Account, (akaunti maalumu) lakini huo ndio umekuwa ni mchezo, juzi hapa tumekuta fedha kiasi cha Shilingi bilioni 26 zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya matumizi ya TRA, zikapelekwa kwenye benki tatu kama Fixed Deposit Account na Bodi ya TRA ikapitisha, ndio maana nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri.
“Hata kwa sasa hivi Waziri (wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako) upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa kwa sababu maalumu, inachangiwa fedha wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye Fixed Deposit Account, Waziri hiyo ni message sent and Delivered,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alisema kumekuwa na mchezo wa wakuu wa taasisi mbalimbali kuchukua fedha na kuziwekwa kwenye akaunti maalumu ambako serikali inakwenda kukopa kwa gharama kubwa.
“Kwa sasa huu ndio mchezo ambao unachezwa na kuisababishia serikali kukosa fedha jambo ambalo serikali haiko tayari kuona matumizi mabaya ya fedha zake,” alieleza Dk Magufuli ambaye anafahamika kwa kusisitiza kubana matumizi ya serikali na kukerwa na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa serikali.
Alisema mchezo huu umekuwa ukiipa serikali gharama kubwa kwa sababu ya kukopa fedha kwenye benki kwa gharama kubwa na kupotosha upatikanaji wa mapato.
“Naomba mtuombee tuendelee kutumbua kwani nchi ilifika mahali pabaya ambapo wanaweza kuitisha vikao hata Ulaya na kutokana na tumbua hii mapato yameongezeka kutoka trilioni 1.2 na kufikia 1.8 ambapo uchumi umeimarika,” alieleza Dk Magufuli.
Alisema uchumi umeimarika na unatakiwa ukue kwa asilimia 7.2, lakini hadi robo ya mwaka huu umekua kwa asilimia 7.9 na kuwa moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi, ambazo kati ya nchi tano imekuwa ya pili baada ya Ivory Coast.
Aidha, alisema thamani ya fedha imepanda na kwamba wanaopotosha juu ya fedha ni wale waliokuwa wanapiga dili ambao kwa sasa hawana nafasi. Jumla ya wahitimu 4,027 walihitimu na kutunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda.
Social Plugin