Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSIBA WA SAMWEL SITTA WAACHA HISTORIA YA AINA YAKE KATI YA WABUNGE WA UPINZANI NA WALE WA CCM

MSIBA wa aliyekuwa Spika wa Bunge la tisa, maheremu Samuel Sitta, umeacha historia ya aina yake kati ya wabunge wa vyama vya upinzani na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sitta ambaye alizikwa juzi katika makaburi ya familia yaliyopo Kitongoji cha Mwenge, nje kidogo ya mji wa Urambo mkoani Tabora, enzi za uhai wake aliongoza Bunge bila kujali itikadi za vyama.

Kwa sababu hiyo aliweza kuandika historia ya kuheshimika kwa wabunge wa vyama vyote, hasa upinzani ambao wakati huo walikuwa wachache bungeni, lakini aliwapa nafasi ya kujibu au kutoa hoja zao.

Ushahidi wa suala hilo ulijidhihirisha wiki iliyopita baada ya kufariki dunia.

Kauli mbalimbali zilizotolewa na wabunge wa upinzani zikidhihirisha jinsi kiongozi huyo aliyekuwa akitumia falsafa ya kasi na viwango, alikuwa akiongoza Bunge kwa kufuata kanuni na taratibu.

Lakini, jambo kubwa ambalo linaonekena wazi kuunganisha wabunge hao ni hatua ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kupanda ndege moja na Naibu Spika wa Bunge,Dk.Tulia Ackson kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa picha zilizopigwa na ofisi ya waziri mkuu juzi, Mbowe na Dk.Tulia walikuwa wamekaa jirani na walikuwa wakiteta mara kadhaa.

Mbowe na Dk. Tulia, kwa kipindi kirefu walikuwa na msuguano hasa wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka huu, baada ya Mbowe na wabunge wa upinzani kutangaza hadharani kuwa hawana imana na Dk.Tulia.

Mbowe na wenzake hao walifikia uamuzi huo baada ya kudai Dk. Tulia anapendelea zaidi wabunge wa CCM wakati wa mijadala ya Bunge.

Kutokana na hali hiyo wabunge hao walikubaliana kutoshiriki vikao vyote vya Bunge anavyoongoza Dk. Tulia.

Pia, siku Dk.Tulia alipopewa nafasi ya kufungua semina ya wabunge kuhusu malengo endelevu ya dunia kwenye ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, wabunge wote wa Ukawa walitoka nje.

Semina hiyo ilikuwa imeandaliwa na Umoja wa Mataifa (UN)kupitia mpango wake wa kufanya kazi pamoja.

Wabunge hao walirejea ukumbini na kushiriki semina hiyo baada ya Dk. Tulia kumaliza kuwasilisha hotuba yake.

Pamoja na tofauti hizo kuanza kupatiwa ufumbuzi hivi karibuni kupitia kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, wakati wa msiba wa Sitta umeonekana kuwaunganisha Wabunge wa upinzani pamoja na Dk. Tulia.

Mbowe na msiba

Mbowe akitoa salamu za Kambi ya Upinzani Bungeni wakati wa kuaga mwili wa Sitta mjini Dodoma, alisema marehemu alikua kiongozi mwenye alama ya umoja na hakuwa mbaguzi.

“Ilifikia mahali tukapata shida ya kutambua kuwa kama bado ni kada wa CCM ama la kwa sababu alimpigania kila aliyemuongoza na alitaka Bunge lisimame kama mhimili.

“Lakini pia, upendo huu umeonekana pia kwa Mama Sitta (mke wa Sitta) kwa kuwa mnyeyekevu kwa sababu kuna kipindi alinifuata ofisini kutaka nimsaidie kuwaunganisha kina mama katika Bunge.

“Hakika, Mungu akujaze faraja,” alimaliza Mbowe.

LISSU

Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema wabunge wamekutana kukumbuka mmoja wa miamba ya Tanzania.

“Ni haki kufanya kumbukumbu hii ndani ya ukumbi wa Bunge ambao aliutawala kwa uhuru na uwazi.

“Katika historia ya Bunge, nchi hii itamkumbuka kwa uongozi wake wa miaka mitano ya kuanzia 2005 hadi 2010.

“Katika kipindi hicho, alifanikiwa kuliondoa Bunge katika kivuli cha utawala wa chama kimoja na kulifanya Bunge kuwa la vyama vingi kama tunaloliona sasa.

“Alilifanya Bunge kuwa lenye meno,lenye uwezo wa kuidhibiti Serikali na hii ndiyo zawadi kubwa ya utumishi wa muda mrefu aliotuachia kama Spika,hakuwa kibaraka wa mtu yeyote.

“Alikuwa mtu mwenye msimamo huru na tunapomkumbuka ni vema tukamkumbuka kwa kujiuliza hili ndilo Bunge alilolitaka?

“Ukijiuliza hivyo, utakuwa umemkumbuka kwa namna inayostahili,”alisema Lissu.

ZITTO

Naye Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema Sitta anayo mengi ya kukumbukwa, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu aliyejaribu kuboresha kila jukumu alilokabidhiwa na pia atakumbukwa kwa sababu alikuwa shujaa wa wote wanaoamini katika uwajibikaji.

“Alikuwa mwanasiasa aliyepanda na kushuka na kubakia kileleni, alikuwa mwana mageuzi wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania.

“Ni mtu wa namna gani wewe Samuel Sitta, Spika wa kasi na viwango, uliyeweka rekodi hata ukiwa umelala kwenye jeneza lililopambwa na bendera ya watu?” alisema Zitto.

Kwa mujibu wa Zitto, Sitta alikuwa kiongozi wa kuliunganisha Taifa kwa sababu ya utendaji wake wa kazi.

“Ulipopokea uspika wa Bunge kama ilivyokuwa ahadi yako, uliliboresha na uliwezesha kutungwa sheria mpya.

“Nakumbuka siku moja ulimuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aongee na baadhi yetu wakati huo mwaka 2006, nilikuwa na miaka 29.

“Tulikutana pale ukumbi wa Msekwa, uliniambia babu mimi sasa niko alasiri ila ninyi ndo saa nne asubuhi na hapa naweka misingi tu. Kilichofuata baadaye ni mabadiliko makubwa ya Bunge,”alisema Zitto.

Aliendelea kusema kuwa marehemu Sitta, alikuwa kielelezo muhimu cha demokrasia kwa sababu alitoa nafasi kwa wabunge wote wa kambi zote.

“Hatusemi ulibagua la hasha, u ccm ulikuwa pale pale! Walio wengi walishinda na walio wachache walisikika, hiyo ndiyo demokrasia,”alisema.

CUF

Mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki ShahaliMngwali, alisema wabunge na watumishi wengi wamebakia kumtaja kwa wema kwa sababu alipokuwa Spika wa Bunge la tisa, aliacha milango wazi kwa watu wote.

Chanzo-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com