Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro |
Mwanamme aliyefahamika kwa jina la Kadami Mwendagiza(34) amemuua mke wake Mwajuma Jange(29) kwa kumkaba shingo kisha naye kujinyonga kwa kutumia kanga katika kijiji cha Ishinabulandi kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Novemba 25 mwaka huu saa 3:30 asubuhi nyumbani kwa wazazi wa mwanamke huyo.
Akielezea kuhusu tukio hilo,Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amesema mwanamme huyo alimuua mke wake kwa kumkaba shingo.
Amebainisha kuwa baada ya mwanamme huyo kumuua mkewe naye aliamua kujiua kwa kujinyonga kwa kutumia kanga na kujitundika katika kenchi ya chumba walipokuwa wanandoa hao.
"Kabla ya tukio wanandoa hao walikuwa na ugomvi wa kifamilia wa muda mrefu hali iliyosababisha wanandoa hao kurudi kutoka Dar es salaam walipokuwa wanaishi na kufikia kwa wazazi wa mwanamke katika kijiji cha Ishinabulandi kujaribu kupata ufumbuzi wa mgogoro wao", ameeleza kamanda Muliro.
"Siku ya tukio wanandoa hawa waliamka salama na wazazi wa mwanamke waliwaacha nyumbani kwenda kufanya shughuli zao za kiuchumi lakini baadae nyuma ugomvk ulianza tena na mwanamme akamuua mkewe na yeye kujiua kwa kujinyonga",ameongeza Muliro.
Kamanda Muliro amesema marehemu wameacha mtoto mmoja Ibrahim Kadami(10) mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Bugijibaga wilaya ya Shinyanga.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin