RAIS Dk. John Magufuli amezungumzia safari yake ya mwaka mmoja wa
urais Ikulu, akieleza mafanikio na changamoto alizozikuta huku akisema
kuna makaburi amelazimika kutoyafukua kwa sababu yanaweza kumshinda
kuyafukia.
Ingawa hakufafanua juu ya makaburi hayo, kauli hii ya sasa inaelezwa
kutoa taswira nyingine mpya ya Rais Magufuli ambaye tangu aingie
madarakani amejipambanua kama mtu aliyekuja kusafisha nchi.
Kauli hiyo aliitoa jana katika mkutano wake na wahariri pamoja na
waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari uliofanyika Ikulu jijini Dar
es Salaam na kurushwa moja kwa moja na televisheni na redio.
Rais Magufuli alilazimika kutoa kauli hiyo wakati akijibu swali
aliloulizwa na mmoja wa waandishi waliohudhuria mkutano huo aliyetaka
kufahamu changamoto alizozikuta katika nafasi aliyoishikilia sasa.
“ Nimeshughulikia changamoto mbalimbali lakini siwezi kuyafukuwa
makaburi yote kwa sababu kuna mengine nitashindwa kuyafunika, sikuja
kufukua makaburi nataka kuanza na yale niliyoyakuta ili tujenge Tanzania
yetu,” alisema.
Katika hilo alisema kazi ya kuiongoza nchi sio nyepesi na hivyo kuwashangaa wale wanaoutaka urais.
“ Nilibeep, ikaita ikajipokea, kazi ya urais sio nyepesi, wanaotaka urais nawakaribisha sana,” alisema Rais Magufuli.
Katika kuonyesha ugumu wa kazi hiyo, Rais Magufuli alisema wakati mwingine analazimika kulala usiku wa manane.
“Nalala saa tisa au saa kumi usiku wakati mwingine” alisema .
Alikwenda mbali na kusema kazi ya kuijenga Tanzania asiachiwe Rais
peke yake hivyo akawataka waandishi wa habari kuhakikisha wanamsaidia
katika kufichua maovu yanayotendeka serikalini.
“Rais hawezi kuona kila kitu lakini ninyi mna jukumu la kuhakikisha
mnafichua maovu na mimi ninasoma kila kitu mnachoandika na mengine
nikiyafuatilia nakuta yana ukweli ndani yake ,” alisema.
KATIBA MPYA
Rais Magufuli pia alizungumzia mchakato uliokwama wa upatikanaji wa Katiba Mpya akisema aachwe anyooshe nchi kwanza.
Licha ya kusema kwamba mchakato huo ulikuwa umefika katika hatua
nzuri lakini yeye binafsi suala la Katiba hakupata kulizungumzia katika
kampeni zake.
“Tutengeneze nchi kwanza, nimezunguka nchi nzima wakati wa kampeni
sikuzungumzia Katiba Mpya kwa hiyo katiba zinaweza kuwa nyingi tu
lakini kwa sasa mniachw ninyooshe nchi kwanza,” alisema Rais Magufuli.
MADUDU MAPYA
Akielezea changamoto alizozikuta ikiwamo ile ya mtandao wa wizi wa
fedha za umma Rais Magufuli alifichua jinsi fedha za serikali
zilivyokuwa zinatafunwa na wapiga dili kupitia mgongo wa benki
mbalimbali hapa nchini.
Alisema baadhi ya wakurugenzi wa mashirika ya Umma walikuwa
wanachukuwa fedha za serikali na kuzipeleka benki kwa mtindo wa
kuzihifadhi kwa njia ya ‘fixed account’ na kisha kuzitumia kufanya
biashara na serikali.
“ Nimekata mirija ya wapiga dili wote, Tanzania inabenki zaidi ya 50,
zote hizi zilimuhudumia mwananchi kwa asilimia 20, kiasi kilichobaki
eti walitegemea kufanya biashara na Serikali.
“ Haiwezekani baadhi ya wakurugenzi walikuwa wanachukua fedha za umma
wanapiga dili na watu wa benki kwa kuziweka fedha hizo kwenye ‘fixed
account’ halafu benki hiyo inazitumia kuikopesha Serikali tena kwa
asilimia 16, nimekata mirija hiyo na hao wapiga dili waendelee kulia
kuzikosa hivyo hivyo hizo fedha,” alisema.
Alisema mbali na wakurugenzi pia baadhi ya wanasiasa walitumia mashirika ya umma na benki hizo kuchota fedha za umma.
Alilitaja Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa ni
miongoni mwa mashirika ya umma yaliyotumiwa na wanasiasa kujichotea
fedha.
“Unamuona mtu anapiga kelele wee, unadhani yuko clean( safi) lakini
unakuta majina yao yapo kwenye madeni… wanakwenda kukopa mabilioni ya
fedha tena bila kulipa, wengine kumbe walikuwa wanaishi bure katika
nyumba za mashirika ya umma bila kulipa kodi lakini ndio wapiga kelele
wakubwa.
“Yalikuwa yakifanyika mambo ya ovyo ovyo tu ya dili, hata ndani ya
CCM wapo watu wa ovyo ovyo wapiga dili, nataka niwaambie bila kufanya
kazi hawataiba hata senti tano,”.
Akizungumzia mtazamo wa watu wanaomuona kuwa anatumia hoja ya maendeleo kuminya demokrasia, Rais Magufuli alipuuza hoja hizo.
“ Hivi karibuni mmesikia chama kimoja cha kisiasa kwenye vikao vyao
vya ndani wanagombana wao kwa wao sasa hiyo demokrasia naiminya vipi?.
Mmeona chaguzi zinaendelea hata hapa wamechagua Ukawa, Lakini pia
tunatakiwa kujua demokrasia ina mipaka yake baada ya uchaguzi watu
waendelee na uzalishaji”.
BARAZA LA MAWAZIRI
Katika kuelezea mafanikio ya mwaka wake mmoja wa urais madarakani,
Rais Magufuli licha kusema zipo changamoto katika Baraza lake la
Mawaziri lakini alisema bado ana imani nalo.
“Serikali niliyounda imenisaidia sana na wanafanya kazi zao vizuri,
niliona niwe na baraza la watu wachache katika kuwatumikia wananchi,”
alisema.
Akizungumzia suala la huduma za afya hususani changamoto ya
kukosekana dawa, alisema katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali yake
ilitenga sh. bilioni 1.99 kwa ajili kununua dawa.
“Tumebadilisha utaratibu badala ya kununua dawa kutoka kwa
wasambazaji sasa tunanunua moja kwa moja kutoka viwandani pia kuna nchi
zinataka kuwekeza hapa nchini kwa kujenga viwanda vya kutengeneza
madawa,” alisema Rais.
Alizungumzia suala la uchumi wa viwanda alisema Watanzania
wasiitegemee Serikali katika kujenga viwanda na kwamba inachofanya ni
kuhamashisha watu binafsi kuwekeza katika eneo hilo.
Pamoja na hilo Rais Magufuli alisema serikali yake imetimiza lengo
lake la makusanyo ya kodi yanayofikia sh. trilioni 1.2 kutoka sh.
bilioni 800.
Alisema katika bajeti ya fedha ya mwaka 2016/17 serikali yake
imetenga asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku ikiwa tayari
imenunua ndege mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400.
Kwa mujibu wa Rais Maguli serikali yake inatarajia ndege nyingine
mbili aina ya Jeti pamoja na Bombardier na mwaka 2018 ataongeza ndege
aina ya Boeing na kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano serikali
itakuwa na jumla ya ndege saba.
Pamoja na hilo Rais Magufuli alielezwa kufurashwa na kasi ya kukuwa kwa uchumi kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia 7.2 sasa.
Alisema kasi hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barania Afrika
nyuma ya Ivory Coast ambao kasi ya uchumi wake inakuwa kwa kasi.
AKWEPA SAFARI 47
Akifafanua dhana ya kubana matumizi, Rais Magufuli alisema kwamba
alianza kwa kujibana mwenyewe ambapo alialikwa safari 47 lakini
amekwenda safari tatu tu.
Alisema safari nyingine aliwakirishwa na mabalozi, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Rais.
“ Unajua kusafiri kwangu lazima niwe na watu zaidi ya 40 lakini
nikiwatuma wengine msafara wao huwa ni wa watu wawili kwa hiyo fedha
nyingi inapona na tunaipeleka kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Rais.
WAFANYABIASHARA
Kuhusu hoja ya serikali kuwatenga wafanyabiashara, Rais Magufuli
alisema serikali yake haijawatenga na kwamba inawahitaji sana na yeye
anawapenda lakini anataka walipe kodi.
“Palikuwa na mambo ya ovyo, sitaki kwenda kwenye details sana maana
mambo mengine yapo mahakamani ila niwaambie ukweli wafanyabiashara
matapeli siwapendi”.
Akifafanua madai kupanda kwa mishahara licha ya wafanyakazi hewa
kuondolewa Rais Magufuli alisema hilo limetokana na madai ya siku za
nyuma ya wafanyakazi ambayo yamesababisha serikali yake kulipa sh.
bilioni 22.6 huku kukiwa bado kukiwa na mengine 39,000 yenye thamani ya
sh. Bilioni 23.
Alisema madai hayo mengi yalitokana na watu waliopandishwa vyeo
kutolipwa fedha zao za kiwango cha nafasi waliyopewa, pia madeni ya
watumishi kwenye mifuko ya jamii ambazo serikali ilikuwa bado
haijawasilisha.
“Ndio maana nilisitisha ajira kwa miezi miwili, kwanza wakati huo
kulikuwa na vijana wako mafunzoni jeshini nilisubiri wamalize mafunzo
yao ili wakiingia kwenye ajira mpya tunaanza pamoja. serikali imeanza
kutoa ajira na hadi leo imeajiri watumishi 5000, wamo madaktari 100 na
tunataraji kuongeza 200 wengine katika hospitali yetu ya Mloganzila,”
alisema.
MAPAMBANO YA UJANGILI/RUSHWA
Kuhusu mapambano dhidi ya ujangili Rais Magufuli alisema Serikali yake imejipanga kuhakikisha inakomesha suala hilo.
Akizungumzia suala la mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi, alisema
matunda kuhusu yameanza kuonekana baada ya nidhamu kurejea makazini.
“ Tumepitisha sheria ya mafisadi na sheria ilivyofika kwangu
nilisaini siku hiyo hiyo, na kesi ya kwanza imeanza kusikilizwa jana
(juzi). Rushwa ni suala myambuka na haliwezi kushughulikiwa na Rais
peke yake . Nitoe wito kwa Watanzania wote tukatae kwa sababu ni kansa
ya maendeleo,” alisema.
Chanzo-Mtanzania
Chanzo-Mtanzania
Social Plugin