Shirika
la uzalishajimali lililo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa (Suma – JKT)
litaanza kutekeleza mpango wa kufuga samaki kwa kutumia vizimba (Cages)
katika bahari ya Hindi baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa
katika mito na maziwa mbalimbali hapa nchini.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuhyo muda mfupi
baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Meja
Jenerali Isamuhyo amesema ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba umepata
mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali nchini hususani katika ziwa
Viktoria na kwamba ili kupanua ufugaji huo Suma-JKT inajielekeza kufuga
samaki katika bahari ya Hindi.
Ameongeza
kuwa pamoja na ufugaji wa Samaki, Rais Magufuli ameliagiza Jeshi la
Kujenga Taifa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na shughuli
zilizotajwa katika misingi ya uanzishaji wa jeshi hilo ili Serikali
isipate gharama za kununua chakula kwa ajili ya vijana wanaokwenda
kupata mafunzo ya JKT na pia kupata chakula cha ziada ambacho kitatumika
kutatua tatizo la uhaba wa chakula katika maeneo yatakayokumbwa na
uhaba.
Meja
Jenerali Isamuhyo ameongeza kuwa Rais Magufuli ameitaka JKT kujenga
mabwawa kwa ajili ya kuanzisha kilimo cha umwagiliaji katika maeneo
yanayofaa kwa kilimo hicho.
Aidha,
Mkuu huyo wa JKT amebainisha kuwa JKT itahakikisha inasimamia
utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais na kuongeza kuwa kazi hii
itakwenda sambamba na utekelezaji wa majukumu mengine ya JKT
yaliyoainishwa katika uanzishwaji wake mwaka 1963 ikiwemo ujenzi kwa
gharama nafuu.
Wakati huo huo,
Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Jenerali
Mstaafu George Marwa Waitara Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Novemba, 2016
Social Plugin