Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Telack kufuatia vifo vya watu 18 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani katika kijiji cha Salala Kilichopo katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini Mkoani Shinyanga tarehe 06 Novemba, 2016.
Ajali hiyo ilitokea Majira ya saa moja jioni baada ya gari dogo aina ya Noah lililokuwa limebeba abiria 21 kugongana uso kwa uso na lori na kusababisha vifo vya watu 18 na wengine 3 kujeruhiwa.
Katika salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa na ajali za barabarani zinazoendelea kutokea na ametaka vyombo vinavyohusika na wadau wa usalama barabarani kushirikiana kukabiliana na ajali hizo.
"Ni jambo linaloumiza na kusikitisha sana kupoteza idadi kubwa ya watu namna hii, nakuomba Ndugu Mkuu wa Mkoa Shinyanga Bi. Zainab Telack unifikishie pole nyingi kwa familia za Marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki waliopoteza jamaa zao na uwaambie tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo" amesema Rais Magufuli.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Jaji Zubeir Juma Mzee kilichotokea jana tarehe 07 Novemba, 2016 Mjini Unguja.
Sambamba na salamu hizo, Rais Magufuli pia amemtumia salamu za rambirambi Dkt. Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kufuatia kifo cha Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Ndugu Saleh Ramadhan Ferouz kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 08 Novemba, 2016 Mjini Unguja.
"Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za viongozi wetu wastaafu waliotangulia mbele za haki hapo jana, tutawakumbuka kwa mchango wao mkubwa kwa Zanzibar na Taifa letu kwa ujumla kwa kuwa katika kipindi chao cha uongozi walijitahidi kutimiza wajibu wao na kuleta manufaa kwa Taifa" amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi. Amina
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
08 Novemba, 2016
Social Plugin