Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI: PENGO LA SPIKA MSTAAFU SAMWEL SITTA NI KUBWA,KAMWE HALITAZIBIKA NDANI YA SERIKALI,CHAMA NA JAMII


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mkewe Mary wakiweka udongo kwenye kaburi la Spika mstaafu, Samuel Sitta katika maziko yaliyofanyika Urambo, Tabora, jana. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

*****
SERIKALI imekiri kwamba pengo la Spika mstaafu, Samuel Sitta ni kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa salamu za Rais John Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan kwenye maziko ya Spika huyo yaliyofanyika kitongoji cha Mwenge, Urambo mkoani Tabora jana.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kama serikali wamepata pigo kwa kumpoteza mtu muhimu serikalini. Majaliwa alisema, kuondokewa na mzee Sitta ni pengo kubwa na kamwe halitazibika ndani ya serikali, chama na jamii kwa ujumla kutokana na mchango wake wakati wa uhai wake.

Pamoja na kutoa pole kwa familia, aliisihi wao pamoja na wana Urambo kwa ujumla kuupokea msiba huo kwa mikono miwili, licha ya ukweli kuwa kifo siku zote huwa hakizoeleki.

Akifafanua zaidi jinsi taifa lilivyonufaika Waziri mkuu huyo alisema, Sitta akiwa mtumishi wa serikali atakumbukwa kwa mazuri yake kwani alikuwa mtumishi aliyetukuka, mpenda amani, msikivu na aliyependa kushirikiana na jamii.

Alisema uongozi wake ulikuwa mfano wa kuigwa na viongozi na jamii kwa ujumla na kwamba kila kazi ambayo alipewa hakusita kuipokea na wala hakuwahi kuishindwa.

Majaliwa alisema binafsi asiwe mchoyo wa fadhila, kwani alimfundisha kazi kipindi ambacho yeye alikuwa mkuu wa wilaya ya Urambo na Sitta akiwa mbunge wa jimbo la Urambo na Spika wa Bunge la Tisa.

“Mara kadhaa alikuwa akikaa nami pale juu ghorofani nyakati za usiku saa mbili na kunifundisha kazi.....lakini alinionya kuwa nisipende kujihusisha na migogoro ya watu na alinitaka kupenda kazi kamwe nisiwe mvivu,” alisema.

Spika wa Bunge, Job Ndugai akimzungumzia Sitta, alisema kwamba Bunge halitasahau mchango wake na kwamba Bunge hilo limeguswa na msiba huo.

Alisema kwa niaba ya wabunge wote anapenda kuieleza familia ya Sitta kuwa wapo pamoja naye katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

Huku akibubujikwa na machozi, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema Sitta alikuwa mahiri katika kazi zake na kwamba WanaTabora walifurahishwa kuwa na mtumishi wa aina hiyo katika maisha yao.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi alisema hakika CCM imempoteza mtu muhimu na kiungo ndani ya CCM. Alisema siku zote Sitta hakuwahi kupewa kazi na chama halafu akashindwa.

Msemaji kambi ya upinzani, Freeman Mbowe alisema wamepoteza mtu ambaye alikuwa anaifariji kambi hiyo na kwamba msiba huo ni mkubwa kwa Taifa la Tanzania.

Mbowe akizungumza aliwakumbusha watanzania kuwa na taifa lenye umoja kwani ni maslahi ya taifa, ndiyo yanawaunganisha kama Sittta walivyowaungabnisha katika msiba huo.

Alisema kipindi hiki Sitta atakumbukwa kwa kazi aliyoifanya na hasa ile akiwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kwani hadi ameondoka Katiba mpya ilikuwa bado kupatikana.

Mbunge wa jimbo la Bukene wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Suleiman Zedi kwa niaba ya wabunge wote wa Tabora alisema wanaungana kwenye msiba huo na kuwaomba wanafamilia kuwa watulivu kipindi hiki cha majonzi.

Serikali Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mohammed Aboud kwa niaba ya rais na watu wa Zanzibar alisema Wazanzibari wote wamepokea kwa masikitiko makubwa na wanaungana na familia hiyo kuwafariji.

Alisema ametumwa kuja Urambo kuungana na familia na wana Urambo wote kuomboleza msiba kwani sisi sote tutaenda huko.

Viongozi wa dini

Awali Askofu Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa ambaye aliongoza misa ya kuaga mwili na maziko, amewataka viongozi wa nchi kumpenda Mungu na Ibada kama Spika mstaafu Samuel Sitta alivyokuwa akipenda ibada na kumtumikia Mungu siku za maisha yake.

Alisema kiongozi mzuri wa wananchi ni yule anayempenda Mungu kwani watu anaowaongoza wameumbwa na Mungu.

Dk Malasusa pia alitoa rai ya viongozi kuendeleza umoja na ushirikiano bila kujali itikadi zao za kisiasa kama walivyofanya katika msiba huo kukusanyika na kushirikiana kwa umoja.

Askofu huyo wa kanisa hilo Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP) aliambatana na maaskofu wengine watano na baadhi ya wachungaji katika ibada hiyo ya maziko akiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Paul Luzoka, Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Maziko

Shughuli za maziko ya Spika huyo mstaafu zilianza saa tatu asubuhi katika viwanja vya shule ya msingi Urambo zikiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyeambatana na mkewe ambapo watu mbalimbali walipata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho.

Wengine waliohudhuria ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni Freeman Mbowe, Spika wa Bunge Job Ndugai,Naibu Spika wa Bunge, Tulia Ackson, Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda, Mawaziri na wabunge.

Shughuli hizo za maziko zilifanyika kwa saa tisa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 11 jioni katika viwanja hivyo vya shule na baadaye katika maeneo ya makaburi ya ukoo wa Sitta yaliyopo kilometa mbili kutoka nyumbani kwake.

Katika maziko hayo, mwili wa Sitta uliingizwa kaburini saa 10:05 jioni na Askari wa Bunge huku ukisindikizwa na Mke wa marehemu, Mbunge wa Urambo, Margareth sitta, mama yake mzazi marehemu Sitta pamoja na watoto wake waliokuwa wameshikilia jeneza.

Baada ya mwili wa marehemu kutumbukizwa katika kaburi lililojengwa na kusakafiwa kwa saruji lilifunikwa kwa mfuniko ya zege na kisha kuwekwa mashada juu yake.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na Siasa, Uledi Mussa alisoma wasifu wa marehemu. Sitta aliyezaliwa mwaka 1942 na kufunga ndoa na Margareth mwaka 1968 na mpaka kifo chake walijaliwa watoto watano.

Pia alizungumzia jinsi Sitta alivyofanya kazi mbalimbali katika utumishi wa umma ikiwemo ya Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) mwaka 1996 mpaka 2005 aliposhika nyadhifa ya Uspika wa bunge la tisa la kasi na viwango.

Alisema katika kipindi hicho Sitta amewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na Iringa na akiwa waziri wa ujenzi ndipo lilijengwa Daraja la Selander na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere (JNIA).

Samuel Sitta alifariki dunia Novemba 7, mwaka huu katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani na mwili wake kuletwa nchini Novemba 10 mwaka huu na kuzikwa jana katika wilaya ya Urambo mkoani Tabora.

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko, Dar na Lucas Raphael, Urambo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com