Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRENI YA ABIRIA YANUSURIKA KUCHOMWA MOTO DAR

TRENI ya abiria  inayofanya safari zake kati ya Kituo Kikuu  cha Reli na maeneo ya Pugu  Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’ nusura ichomwe moto juzi, baada ya wananchi   kudai kuchoshwa na usumbufu wa shirika hilo.

Wananchi hao walitaka warudishiwe nauli zao  kwa kile walichodai Shirika   la Reli Tanzania (TRL)  limeshindwa kuwa na ratiba inayoeleweka.

Tukio hilo lilitokea juzi  saa 3:00 usiku eneo la Majumbasita, baada ya treni hiyo kukaa kituoni hapo kwa muda mrefu bila kuambiwa kuambiwa chochote.

Hali hiyo iliwafanya abiria  kuvamia kituo kidogo cha mawasiliano kilichopo eneo hilo wakitaka warejeshewe  nauli zao vinginevyo wangekichoma moto pamoja na mabehewa ya treni hiyo.

Mwandishi aliwashuhudia abiria   wakitaka kuingia ndani ya kituo hicho huku wakiwalazimisha wafanyakazi waliokuwapo wawarudishie fedha zao za nauli.

Purukushani hiyo iliyodumu kwa takribani saa  mbili  ilimalizika kwa abiria hao kuvunja vioo vya mabahewa ya treni vipatavyo 30.

Wafanyakazi kuona hivyo walijifungia ndani ya kituo hicho  huku  polisi  waliokuwa wakisindikiza treni hiyo  wakitimua mbio   kunusuru  maisha yao.

Baadhi ya abiria walisema   tangu Ijumaa   iliyopita wamekuwa wakipata usumbufu kwa kukatishiwa tiketi huku treni  ikichelewa na wakati mwingine kutoonekana  kabisa.

Walisema  jambo hilo  limekuwa likiwasababishia hasara na kuwalazimu  kutafuta usafiri mwingine na   kuchelewa kufika  kwenye  majukumu yao.

Kufuatia kukithiri vitendo vya uharibifu wa miundombinu ya reli na treni vinavyofanywa na baadhi ya wananchi, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kupitia  kwa Mkurugenzi Mtendaji , Masanja Kadogosa imetoa onyo kwa wananchi kutofanya vitendo hivyo.

“Tukio hili si mara ya kwanza kujitokeza, lilijitokeza tarehe 24, 26 na 28 mwezi wa 10 na Novemba 7 Katika matukio hayo kulitokea uharibifu wa miundombonu na kujeruhi baadhi ya wafanyakazi wa TRL akiwemo Mustapha Omary ambaye ameshonwa nyuzi 8 katika hospitali ya mnazi mmoja,” amesema.

Amesema kutokana na uharibifu huo, watuhumiwa 17 wanashikiliwa na jeshi la polisi na kwamba upepelezi ukikamilika watachukuliwa hatua za kisheria.

Kadogosa amedai kuwa, wahusika wa fujo na uharibifu huo ni makondakta wa dalala kwa lengo la kutisha wananchi kutoutumia usafiri wa treni.

“Kuna watu wa daladala wanafikiri wataendelea kufanya fujo ili wananchi waone kuwa usafiri wa treni si salama wapande magari yao, sisi hatulazimishi wananchi kuutumia usafiri wetu ila kutokana na ubora wa huduma zetu wanakuja wenyewe. Pia hatusitishi kutoa huduma kwa sababu ya fujo zao sababu tutawatesa abiria wetu zaidi ya 21,000,”

Naibu Kamishna wa Polisi na Kamanda wa Reli, Simon Chillery amesema jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini wengine waliohusika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com