Baadhi ya Viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar wametakiwa kuacha tabia ya kutumia mitandao ya kijamii kujadili masuala yanayohusu Chama badala yake watumie vikao halali vinavyotambuliwa na Katiba ya Chama hicho.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai wakati akifunga Mkutano wa Viongozi wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja Kichama uliofanyika katika Shule ya Msingi Makunduchi Mkoani humo.
Alifafanua kwamba tabia hiyo ya kujadili, kukosoa na kuwatuhumu baadhi ya viongozi wa ngazi mbali mbali wa Chama na Jumuiya zake kupitia Mitandao ya kijamii ni utaratibu unaokwenda kinyume na miongozo ya chama hicho.
Alisema Katiba ya CCM inaelekeza Kwamba mambo yote yanayogusa maslahi mapana ya Chama yajadiliwe Katika Vikao halali vinavyotambuliwa na kanuni za Chama, kwani jukwaa hilo ndiyo sehemu rasmi ya kukosoana na kupeana maelekezo.
Vuai alisikitishwa na tabia hiyo na kueleza kuwa njia pekee ya kumaliza Changamoto hiyo ni Wanachama na Viongozi kujenga utamaduni wa Kusoma na kuelewa Kanuni, Katiba na miongozo mbali mbali ya CCM ili kufahamu wajibu, majukumu, haki na maadili yanayoongoza Chama.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikifanyika katika Magroup ya Mitandao ya kijamii zikiwemo Facebook, WhatsApp na mitandao mingine, jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa kanuni za Chama.
“ Wanachama, Viongozi na Watendaji naomba muelewe kwamba hiki Chama kinaendeshwa kwa utaratibu maalum ulioelezwa Kikatiba , Kikanuni na miongozo mbali mbali, kwa nia ya kulinda hadhi na heshima ya Chama chetu, na hakuna jambo lolote linaloshindikana kupatiwa ufumbuzi kupitia utaratibu huo.
"Sasa panapojitokeza baadhi ya Watu miongozi mwetu wakaanza kujadili na kuwakosoa wenzao nje ya mfumo huo basi hao tunawahesabu kuwa wana nia ya kuanzisha Majungu, Fitna na mpasuko katika taasisi yetu.”, alieleza Vuai na Kuongeza kuwa CCM ni Chama imara na kinachoheshimu Demokrasia katika kujadili mambo yake na kuyatolea maamuzi stahiki katika Vikao rasmi na sio vichochoroni au vibarazani.
Aliongeza kuwa sio kwamba kuna viongozi na wanachama wanaogopa ama hawataki kukosolewa lakini lazima heshima na nidhamu iwepo katika kutekeleza matakwa ya Demokrasia ndani ya Chama hicho kwa kuheshimu utaratibu uliowekwa Kikatiba.
Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho ya mwaka 2015/ 2020 katika Mkoa huo aliwapongeza Viongozi wa Majimbo wakiwemo wabunge, wawakilishi na Madiwani huku akiwasisitiza Viongozi wa Chama kuhakikisha wanakagua kikamilifu miradi inayotekelezwa na viongozi hao ili kujiridhisha kama inawanufaisha wananchi wote.
Aliwataka viongozi wa Chama na Jumuiya zake kuwa wa kwanza kutambua kero na changamoto za wananchi wa maeneo mbali mbali na waziwasilishe kwa Wakuu wa Wilaya (DC) ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na Serikali.
“ Huu sio wakati wa kusubiri taarifa zinazohusu Changamoto za Chama, Jumuiya na Serikali ziletwe Ofisini, badala yake mtoke na kuzitafuta wenyewe ili kuwasaidia wanachama na wananchi kutatuliwa kero zao kwa haraka kupitia Mamlaka husika.”, alisisitiza Vuai.
Alisema Viongozi wanatakiwa kufahamu kwamba suala la kuwatumikia wananchi sio jambo la hiari bali ni lazima watekeleze kwa vitendo ahadi walizotoa wakati wa kampeni kwani wasipotekeleza Wajibu wao vizuri kwa jamii mwisho wa siku kitakacho hukumiwa ni Chama na sio kiongozi husika.
Aidha aliwakumbusha viongozi hao kwamba Chama na Jumuiya zake wanatarajia kufanya Uchaguzi mwaka 2017, hivyo waanze mapema kuwaelimisha, kuhamasisha na kuwaandaa kisaikolojia wanachama wa Chama hicho juu ya matumizi sahihi ya kanuni za UChaguzi ili kuepuka lawama zisizokuwa za lazima.
Alisema Wanachama wanatakiwa kuwachagua viongozi wenye sifa na wasiokuwa na Mukhari( kuoneana haya) katika kusimamia mambo ya msingi ya CCM na waumini wa kweli wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Serikali mbili wenye vigezo hivyo ndio wanaofaa kuwa viongozi.
Hata hivyo aliwapongeza Rais wa Zanzibar, Dkt. Shein na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli kwa juhudi na kasi zao za kufanikisha mipango ya maendeleo ya nchi kwa ufanisi mkubwa hali inayoongeza hamasa kwa jamii kuendelea kuwaamini.
Social Plugin