WANAWAKE wawili wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na shambulizi lililosababisha kifo cha aliyekuwa Diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Igagala, Alexander Pugwi.
Washitakiwa hao, Ashura Jafari na Salma Bakari walidaiwa kutenda kosa hilo Novemba 12, mwaka huu, katika eneo la Majengo ya Tabora wilayani Urambo.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa wilaya hiyo, Hassan Momba, ilidaiwa kuwa washitakiwa kwa pamoja siku hiyo, saa 8:00 usiku walimuua Pugwi kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali.
Upande wa mashitaka ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, Philbert Pimma, uliiambia mahakama hiyo kuwa washitakiwa hawatakiwi kujibu lolote kwani shauri lao linapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu, hivyo limepangwa kutajwa Novemba 29, mwaka huu.
Siku ya tukio, Pungwi ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Igagala inadaiwa alifika mjini Urambo akitokea kijijini kwake ili kuhudhuria maziko ya aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta aliyezikwa Jumamosi ya Novemba 12, mwaka huu.
IMEANDIKWA NA LUCAS RAPHAEL-HABARILEO URAMBO
Social Plugin