TAIFA limekumbwa na vilio na simanzi kutokana na vifo vya kufuatana vya viongozi waandamizi, akiwamo Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta na aliyekuwa Waziri wa Elimu na Ufundi, Joseph Mungai, vilivyotokea wiki hii.
Sitta alifariki dunia Novemba 7, mwaka huu, nchini Ujerumani, alipokwenda kutibiwa katika Hospitali ya Technical University of Munich na anatarajiwa kuzikwa leo Urambo, mkoani Tabora, huku Mungai naye akifariki dunia Novemba 8, mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Mafinga, mkoani Iringa.
ZITTO NA MWAKYEMBE
Baada ya mwili wa Sitta kuagwa asubuhi katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana, pia ulipelekwa kuagwa bungeni mjini Dodoma jana, huku wabunge na wageni mbalimbali wakishindwa kujizua na kujikuta wakibubujikwa na machozi.
Shughuli ya kuagwa iliongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, baada ya mwili wa Sitta kuwasili katika viwanja vya Bunge saa 8:50 mchana, ambapo wapambe wa Bunge na maofisa wa Serikali waliokuwa wakiratibu waliuchukua saa tisa alasiri na kuuingiza ndani ya Ukumbi wa Bunge.
Viongozi mbalimbali nao walihudhuria, akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na mkewe, Tunu, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela, wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki na wananchi wengine walioingia bungeni kwa kibali maalumu. Baada ya mwili huo kuwasili, Ndugai alianza kwa kuongoza shughuli hiyo kwa kuanza kwa kuimbwa wimbo wa Taifa na baadaye kutoa salamu kutoka kwa wawakilishi wa vyama vyote vilivyopo bungeni.
Aliyekuwa wa kwanza kutoa hotuba alikuwa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) na alielezea namna Sitta alivyoliongoza Bunge la tisa na kuweka misingi imara ya demokrasia kwa vyama vyote.
Alisema Sitta anayo mengi, lakini Tanzania itamkumbuka kama mtu aliyejaribu kuboresha kila alichokabidhiwa kama jukumu, shujaa wa wote wanaoamini katika uwajibikaji wa kitaasisi, mwanasiasa aliyepanda na kushuka na kisha kupanda na kubakia kileleni.
“Mwanamageuzi wa Bunge na Spika wa mioyo ya Watanzania. Hata katika kifo chake, Sitta ameweka rekodi nyingine kwa Bunge kufanya kikao maalumu kuenzi mmoja wa wajumbe wake mahiri kati ya mwaka 1975 – 2015, isipokuwa tu kwa kipindi cha mwaka 1995 – 2005. Rekodi hii itaendelea kwa wengine wote watakaofuata baada yake,” alisema Zitto na kuongeza:
“Ni mtu wa namna gani wewe Samuel Sitta? Spika wa Kasi na Viwango, unayeweka rekodi hata ukiwa umelala ndani ya jeneza lako lililopambwa na Bendera ya Taifa letu ukielekea nyumbani kwako Urambo katika nyumba yako ya milele. Ulikuwa hushindwi ukiwa hai, umeonyesha umahiri wako hata ukiwa kwenye umauti. Kweli wewe ni Spika wa Watu (The Peoples Speaker).
“Tuliokupenda tunajua. Ulikuwa baba mlezi. ulikuwa mume mwema. Ulikuwa babu. Ulikuwa kiongozi nadhani hata kwa uliokwaruzana nao hapa na pale wanajua hilo. Leo sote tuna majonzi makubwa. Umeliunganisha Taifa katika kukukumbuka ewe Spika wa watu.
“Lakini wala tunakuita Spika Sitta tu kwanini? Kwa sababu legacy yako (urithi) ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Si kwamba umeanzisha Bunge wewe, la hasha. Lakini ulipopokea uspika wa Bunge letu, kama ilivyo jadi yako, uliliboresha, uliwezesha kutunga kanuni mpya, uliimarisha mhimili huu na kuuweka katika nafasi yake ya Kikatiba.
“Nakumbuka siku moja ulimwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aongee na baadhi yetu, ilikuwa mwaka 2006. Mimi nikiwa nina miaka 29 tu. Tukakutana na Rais ukumbi wa Msekwa. Baada ya kikao kilichofanikiwa kumshawishi rais kuhusu mabadiliko uliyoyataka uliniambia babu, mimi sasa alasiri, ninyi ndiyo saa nne asubuhi.”
Kutokana na kauli hiyo, alisema Sitta anaweka misingi na kuliweka Bunge katika nafasi yake ya kikatiba, jambo lililoendana na mabadiliko makubwa ya Kanuni za Bunge kwa kuandikwa upya kwa Sheria ya Bunge ya mwaka 2008, ambayo pia ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo (CDCF).
Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, aliyeendesha dua kwa niaba ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), alieleza namna alivyomfahamu Sitta na alivyomsaidia katika hatua mbalimbali za kimaisha.
“Nasimama mbele ya umati kushukuru kwa ajili ya Samuel Sitta kwa kumpa kipaji kikubwa cha uongozi, ulimpa kipaji cha kuwatumikia na kuwaongoza watu wako. Kwa uadilifu, unyenyekevu, ujasiri wa hali ya juu, ni wewe Mungu ulimpa moyo wa kutetea wanyonge na kuwapigania na kupambana na wale wote waporaji wa rasilimali za Taifa na kila alipopita aliacha alama za uongozi uliotukuka na Bunge hili linashuhudia kazi aliyoifanya Sitta, niseme nini?” alisema.
Dk. Mwakyembe aliendelea kutoa maneno yaliyowafanya wabunge na baadhi ya waombolezaji kuangua kilio.
“Tungeomba Mungu Samuel aendelee kuwa hai lakini umempenda zaidi, umechuma ua la uwaridi, mimi ni mmoja ya Watanzania wengi waliopendelewa na kusaidiwa kwa kila hali na marehemu Sitta, uliyempa mkono wa kutoa moyo wenye mapenzi ya hali ya juu,” alisema Sitta.
Pia alisema Sitta alimfundisha siasa ambapo alimuambia: “Mdogo wangu siasa si sayansi…kwa hiyo mdogo wangu jioteshee ngozi nene ili ukienda juu usiathirike na joto na ukishuka chini usiathirike na baridi,” alisema Dk. Mwakyembe.
LISSU
Naye Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alisema kuwa wabunge wamekutana kukumbuka mmoja wa miamba ya Tanzania.
“Ni haki tunafanya kumbukumbu hii ndani ya ukumbi wa Bunge ambao aliutawala kwa uhuru na uwazi. Katika historia ya Bunge nchi hii itamkumbuka kwa uongozi wake wa miaka mitano (2005-2010) aliofanikiwa kuliondoka Bunge katika kivuli cha utawala wa chama kimoja na kulifanya Bunge la vyama vingi tunaloliona sasa.
“Alilifanya Bunge kuwa lenye meno, lenye uwezo wa kuidhibiti Serikali, hii ndiyo zawadi kubwa ya utumishi wa muda mrefu aliotuachia kama Spika kwa sababu pia hakuwa kibaraka wa mtu yeyote.
“Alikuwa mtu mwenye msimamo huru, hivyo tunapomkumbuka ni vema tukamkumbuka kwa kujiuliza hili ndilo Bunge alilolitaka? Ukijiuliza utakuwa umemkumbuka kwa namna inayostahili,” alisema Lissu.
NDUGAI
Kwa upande wake, Ndugai, alielezea mambo mbalimbali Sitta aliyofanikiwa kuyabadilisha, huku akibainisha namna Mungu alivyomrudisha ili kufanya aliyoacha.
“Hivi karibuni niliugua sana, niliugua hadi kwa akili ya kawaida nikajiuliza kwanini Mungu amenirudisha? Ila sasa katika maombi ya Mungu amenirudisha ili na mimi nitende angalau aliyoyafanya Mzee Sitta,” alisema Ndugai.
Alisema Sitta atakumbukwa kwa kulifanya Bunge la tisa kuwa la mabadiliko, maboresho na hata kuliendesha kwa misingi ya haki, kasi na viwango.
Alisema alikuwa mlezi wake katika nafasi mbalimbali za kuliongoza Bunge, kwa sababu licha ya kuwa nahodha, alimpa nafasi ya kujifunza.
“Tulikuwa wenyeviti watatu, mimi, Jenister Mhagama na Zubeir Maulid Zubeir, ambaye sasa ni Spika wa Baraza la Wawakilishi- Zanzibar, hivyo tunaweza kuona namna gani alivyotulea na najisikia fahari kwa fursa aliyotupatia.
“Nakumbuka mwaka 2006 aliunda Tume ya Bunge ya kuhuisha kanuni, mimi nikiwamo, ambapo aliwezesha kwanza wimbo wa taifa kuanza kupigwa wakati wa kuanza Bunge na kumaliza, kuanzisha utaratibu wa maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu, kamati za fedha kuongozwa na wapinzani ili kujenga demokrasia.
Baada ya shughuli hiyo kukamilika Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitoa hoja ya kuahirisha Bunge hadi Januari 31, mwakani.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema Taifa limempoteza Sitta, aliyekuwa kiongozi mkubwa na shupavu aliyeweza kuandika historia yake mwenyewe iliyosababishwa na utumishi uliotukuka.
Kairuki alikuwa akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali wakati Sitta akiagwa Dar es Salaam, katika shughuli iliyohudhuriwa na Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. John Kijazi, Rais mstaafu Jakaya Kikwete na mkewe, Salma Kikwete, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na mkewe Anna Mkapa, Makamu wa Rais mstaafu, Dk. Gharib Mohamed Bilal, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na Jaji mstaafu Joseph Warioba.
“Aliweza kuandika historia yake mwenyewe, watu wachache wenye uwezo huo waliojaliwa vipawa, karama na fursa kama alivyo Sitta, kwa fikra zake, uongozi wake na kazi za mikono yake ameweza kufanya mambo mengi yenye manufaa kwa nchi na kutuachia alama,” alisema Kairuki.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam, Paul Makonda, alimwomba Magufuli kuwapo kwa eneo maalumu la kuzikia viongozi waliofanya mambo makubwa katika nchi.
“Kwa kuwa Serikali inahamia Dodoma tunaomba kutengwe eneo, ikiwezekana la kuzikia viongozi walioifanyia nchi mambo makubwa na hapo baadaye hata mwili wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tunaweza kuuhamishia hapo,” alisema Makonda.
Makonda, aliyekuwa akilia kwa uchungu muda wote wakati wa kuagwa mwili wa Sitta, pia alisema atamkumbuka kwa kuwa ndiye aliyemsaidia katika kulipa ada alipokuwa akisoma shule ya sekondari mkoani Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Sumaye, alisema Watanzania wanatakiwa kumuenzi Sitta kwa vitendo na si kwa maneno.
“Sitta alikuwa mwadilifu, mchapakazi, mwenye busara, mpigania haki na aliyesimamia alichokiamini, hivyo tunatakiwa tubaki navyo hivi,” alisema Sumaye.
Naye Msemaji wa Familia, Caroline Sitta, aliishukuru Serikali pamoja na viongozi mbalimbali kwa kipindi chote walichokuwa wakimuuguza, huku akisisitiza kuwa enzi za uhai wa baba yake alikuwa akipenda kusaidia watu bila malipo.
“Kwetu alikuwa babu, mume na baba mwenye upendo mkubwa, alipenda kusaidia watu wapate mafanikio bila malipo, alikuwa akikumbuka siku zote za kuzaliwa za watoto na wajukuu,” alisema Caroline.
Mbali na kifo cha Sitta, viongozi wengine waliofariki dunia Novemba 8, mwaka huu na kuzikwa Zanzibar ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jaji Zubeir Maulid, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Salehe Ramadhan Ferouz na Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidh Ali Tahir, aliyefariki dunia mkoani Dodoma usiku wa kuamkia jana na kuzikwa Zanzibar jana hiyo hiyo na kuifanya wiki hii kuwa ngumu kwa Taifa.
Pia watu wengine 19 walifariki dunia kutokana na ajali ya gari aina ya Toyota Noah na lori aina scania iliyotokea usiku wa Novemba 6, mwaka huu katika Kijiji cha Nsalala, mkoani Shinyanga.
Awali akitoa taarifa ya msiba bungeni asubuhi jana, Ndugai, alisema Tahir alifariki dunia kutokana na maradhi ya moyo yaliyokuwa yakimsumbua.
Taarifa hiyo aliitoa baada ya sala ya kuliombea Bunge, nchi na Rais na Ndugai alisema Tahir amekumbwa na umauti saa nane usiku wa kuamkia jana.
“Waheshimiwa wabunge, kuna masikitiko makubwa nawatangazia msiba wa mwenzetu Hafidh Ali Tahir, aliugua ghafla jana (juzi) saa nane usiku na alikwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na alipimwa na kubainika kuwa ana tatizo la moyo na shinizo la damu na madaktari wakiwa wanampatia matibabu alifariki dunia muda mfupi,” alisema Ndugai.
Baada ya taarifa hiyo, ukimya ulitokea bungeni, huku baadhi ya wabunge wakishindwa kujizuia na kububujikwa na machozi kutokana na msiba huo.
Licha ya kutoa tangazo hilo, Ndugai alikuwa akizungumza kwa sauti ya chini yenye huzuni, huku kila jambo alilokuwa akiwahoji wabunge aliitikia nao pamoja.
Ndugai alisema walikuwa na Tahir hadi juzi usiku katika kikao cha Bunge Sports Club, lakini hakuwa na dalili za kuumwa.
Pia alisema Tahir alishiriki katika semina mbalimbali na wabunge wenzake iliyofanyika New Dodoma Hotel.
“Mheshimiwa Tahir alikuwa ni mmoja wa wabunge walioomba kwenda Urambo katika mazishi ya Sitta, tumeondokewa na mbunge mchapakazi, mcheshi, mwanamichezo na aliyewajali wapiga kura wake,” alisema Ndugai kwa huzuni.
Alisema kwa mujibu wa kanuni ya Bunge 152, inayelekeza kwa kusema kuwa inapotokea mbunge atafariki wakati wa Bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili maombolezo na katika hatua nyingine, alisema nusu ya posho ya wabunge ya siku ya jana itatolewa kama rambirambi kwa msiba wa Sitta na Tahir.
Kutokana na hali hiyo, alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama, kutengua kanuni ili kuruhusu shughuli iliyopangwa kufanyika katika kikao maalumu cha kumuaga Sitta na Tahir.
Pia alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Andrew Chenge, kuhitimisha hoja yake ya taarifa ya utendaji kazi ya kamati yake iliyowasilishwa juzi ili ikafanyiwe kazi na Serikali.
Baada ya kutengua kanuni hiyo, Chenge alihitimisha kwa muda mfupi hoja yake bila kuchangiwa na wabunge, tofauti na utaratibu mwingine unaofanyika bungeni.
“Mheshimiwa Spika, siku ya leo (jana) ilikuwa nzito katika historia ya Bunge letu na haijawahi kutokea. Haijawahi kutokea mambo mazito kwa wakati mmoja kama leo hii (jana) tunapokosea hapa na pale naomba tuvumiliane,” alisema Chenge.
Baada ya Chenge kumaliza kuhitimisha hoja ya kamati yake, Ndugai alisitisha kwa kuahirisha shughuli za Bunge saa 9:30 asubuhi hadi saa 08:40 mchana jana, ili kupata muda wa kuaga mwili wa Tahir na baadaye kuaga mwili wa Sitta.
“Basi tuyashike yale yanayotuunganisha zaidi, tuwe na upendo, tuwe ni watu wenye kushirikiana. Upande wa bunge Mheshimiwa Mussa Zungu atamuwakilisha spika na ataambatana na baadhi ya wabunge wa kutoka Zanzibar na bara,” alisema Ndugai.
MAJALIWA
Akitoa salamu za Serikali, Majaliwa alisema ni jambo la kushtua kwa kuwa juzi Tahir alishiriki mambo mbalimbali ya kijamii na kibunge na enzi za uhai wake alijali na kuthamini mchango wa wenzake.
“Leo (jana) tunazungumza akiwa katika hali nyingine, ni jambo la huzuni kwetu na ni funzo kwetu pia, Serikali kupitia Rais Dk. John Magufuli inatoa salamu za pole kwa spika, wafiwa wote, wabunge tupo katika hali ngumu, tumepoteza wabunge wenzetu tuliokuwa nao katika bunge,” alisema Majaliwa.
Pia aliwaasa wabunge wote kutambua safari ya kifo ni ya kila mwanadamu, hivyo ni vyema kujenga na kuimarisha upendo miongoni mwao kwa kuishi pamoja na kushirikiana kwa hali na mali.
“Binafsi mimi nimemfahamu Tahir, nimewahi kuhudhuria naye kozi ya kimataifa ya uongozi katika mchezo wa mpira wa miguu kule Zanzibar mwaka 1996, natambua namna ambavyo alipenda majukumu yake, aliwapenda wenzake na kushirikiana nao. Tuendelee kumuombea kila mmoja kwa dini yake,” alisema Majaliwa.
Alisema Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ndiye atakayeiwakilisha Serikali katika mazishi ya Tahir.
MBOWE
Naye Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema msiba huo uwe somo kwa wabunge wote kwa kuwataka kupendana na kuheshimiana.
Social Plugin