BABA ADAIWA KUMLAWITI MWANAE WA KIUME

Mwanamume mwenye miaka 45 Yohana Omari anatafutwa na Polisi kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 16, kwa zaidi ya miaka miwili. 

Omari ametoroka baada ya kupata taarifa kuwa anatafutwa na wananchi kutokana na tukio alilokuwa akimfanyia kijana huyo (jina linahifadhiwa) tangu mwaka 2013. 

Akizungumzia tukio hilo, kijana huyo alisema kuanzia mwaka huo, akiwa darasa la nne amekuwa akifanyiwa kitendo hicho na baba yake na kukatazwa asiseme. 

Alisema siku ya kwanza alipobaini anafanyiwa ilikuwa usiku akiwa amelala, alishtuka kutokana na kuhisi maumivu makali na kumkuta baba yake amemlalia juu. 

Alifafanua kuwa kuanzia hapo hayo yakawa ndiyo maisha yake na anapolalamika hukosa baadhi ya huduma, jambo lililokuwa likimlazimu akubali kuendelea kwa shingo upande.

 “Kuna mafuta huwa ananipaka na kunifanyia kitendo hicho, nimeishi kwa tabu ikiwamo kuamka asubuhi nimechoka na sina hamu ya jambo lolote, natamani kulala. 

“Imefikia mahali natoka majimaji hadi kuogopa kujichanganya na wenzangu,” alisema kijana huyo.

Kijana huyo alisema kabla ya kuishi na baba yake, alikuwa anaishi na mama yake, lakini alipata mwanamume akaolewa kwa sharti la kutokuishi na yeye, ndipo akampeleka kwa baba yake. 

Alieleza kuwa licha ya kuwaeleza ndugu wa familia, wakiwamo bibi zake, hakuna walichomsaidia. 

“Nimemaliza darasa la saba, nimechaguliwa kujiunga sekondari, lakini sina uhakika wa kuendelea na masomo. 

“Baba amekimbia na kuna viashiria alitumia rushwa, ulinzi shirikishi badala ya kumkamata walimtorosha,” alisema. 

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kwa Mustapha Pugu, Dar es Salaam, Bahati Omari alisema baada ya kupata taarifa hizo, kwa kushirikiana na vijana wake, walifikisha taarifa polisi ili akamatwe lakini alikuwa ameshatoroka. 

Askari polisi mmoja wa eneo hilo alisema baada ya kupokea malalamiko hayo, walimpeleka hospitali kijana huyo kumfanyia vipimo ambavyo alibainisha kuwa amefanyiwa kitendo hicho mara nyingi. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema suala hilo lipo chini ya upelelezi. 

“Tumepokea hayo malalamiko, tunayachunguza kwa sababu yanachanganya, amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo tangu mwaka 2013 na amekuja kubainisha leo, hivyo inahitaji upelelezi wa kina,” alisema Hamduni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post