WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo
kufanya uchunguzi na kumpelekea taarifa ya watendaji waliohusika katika
ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa mradi wa hospitali ya wilaya ya
Monduli uliogharimu sh. bilioni 2.7.
Ametoa
agizo hilo jana (Jumapili, Desemba 4, 2016) wakati akizindua hospitali
ya wilaya ya Monduli ambayo katika ujenzi wake kulitakiwa kuwe na jengo
la maabara ambalo halipo na fedha zimeisha.
"Mkuu
wa Mkoa shirikiana na Sekretarieti yako kufanya uchunguzi na
atakayebainika kuhusika kwenye ubadhirifu huu achukuliwe hatua za
kisheria kwa sababu ujenzi huu ulihusisha na jengo la maabara lakini
tayari mradi umekamilika na hakuna jengo la maabara," alisema.
Naye
Mkuu wa mkoa huo Bw. Gambo alisema tayari wameanza kufanya uchunguzi wa
ujenzi wa mradi huo baada ya kubaini kuwa umetumia kiasi cha fedha
kilichotumika hakilingani na thamani ya mradi huo.
Mkuu huyo wa Mkoa aliahidi kufuatilia suala hilo na uchunguzi utakapokamilika taarifa hiyo itapelekwa kwa Waziri Mkuu.
Awali,
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Zaveri Benela akisoma taarifa ya
hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto ya jengo la upasuaji karibu na
wodi ya wazazi hali inayowalazimu kuwasafirisha wagonjwa umbali wa zaidi
ya mita 300 hadi kwenye jengo la upasuaji lililopo katika majengo ya
zamani.
Pia
kukosekana kwa jengo la wagonjwa wa nje na jengo la maabara kwenye
majengo hayo mapya hali inayochangia huduma kutolewa kwenye maeneo
miwili tofauti kwa wakati mmoja yaani katika wodi mpya na majengo ya
zamani na hali hivyo inaleta usumbufu kwa wagonjwa.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu ametoa siku saba kwa Mkuu wa Wilaya ya
Monduli, Bw. Idd Kimanta kumaliza tatizo la mgogoro wa ardhi katika
kijiji cha Emairete kilichopo Monduli juu mkoni hapa baada ya kudumu
kwa miaka 20.
Mgogoro
huo ni wa shamba kubwa ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya
bia ya Breweries na kisha kurejeshwa kwa kijiji hicho ambapo viongozi
wa zamani wa Kijiji hicho walijimilikisha kinyemela.
Waziri
Mkuu alitoa agizo hilo baada ya kusimamishwa na wanakijiji hao
waliokuwa wamebeba mabango ya kumuomba msaada wa kutatuliwa kwa
mgogoro huo wakati anatoka kudhuru kaburi la Waziri Mkuu wa zamani
Hayati Moringe Sokoine.
Waziri
Mkuu alimtaka mkuu huyo wa wilaya kueleza sababu za kwa ya nini uongozi
wa wilaya umeshindwa kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ambaye alifika
kijijini hapo na kutoa maelekezo.
Baada
ya maelekezo hayo Waziri Mkuu aliwataka wananchi hao kuendelea kuwa na
imani ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dk.
John Magufuli ambayo ipo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hasa wanyonge.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya hiyo alikiri kuwepo kwa mgogoro huo kwa
miaka 20 na kwamba Waziri Lukuvi alitoa maelekezo ambayo halmshauri
inayafanyia kazi na imeshindwa kuleta majibu kwa wananchi hao kutokana
na ziara ya Waziri Mkuu ambaye aliwataka watekeleze majukumu yao na
wasitumie ziara yake kama kisingizio.
Katika
hatua nyingine Waziri Mkuu alisema Serikali na Watanzania wote
wanatambua na kuiheshimu kazi nzuri iliyofanywa na hayati Sokoine kwa
Taifa kipindi cha uhai wake na itaendelea kuienzi. Pia Serikali
itaendelea kushirikiana na familia katika mambo mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Social Plugin