Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BODI YA MIKOPO KUWAANIKA KWA PICHA WADAIWA SUGU,UHAKIKI KUFANYIKA KILA OFISI


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuanzia mwanzoni mwa Januari mwakani, itaanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa sugu kwenye vyombo vya habari waliohitimu katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kuanzia wale wa miaka 10 iliyopita.

Bodi hiyo ilitoa muda wa zaidi ya siku 30 unaoisha kesho Desemba 30, mwaka huu, kwa wadaiwa hao sugu kulipa madeni yao ndani ya muda huo, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kulazimika kulipia gharama za kuwasaka na kuendesha kesi.

Pamoja na hayo, bodi hiyo pia kupitia Sheria ya Bodi ya Mikopo iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni na Bunge, imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kwa kuunda kikosi kazi cha kuhakiki waajiriwa wasiowasilisha makato na majina ya waajiriwa waliokopa HESLB, na adhabu yao itakuwa ni faini au kifungo cha miezi 36 jela.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, alisema baada ya kuisha kwa muda huo wa siku 30 walioutoa, wadaiwa wote sugu, ambao mpaka sasa hawajajisalimisha wenyewe kwa hiari, kulipa madeni yao wataanikwa hadharani na picha zao.

“Tumeamua kuchukua hatua hii ambayo tunaamini itasaidia watu kuwatambua wadaiwa hawa wa bodi, na kuturahisishia kupata taarifa zao na kuwasaka ili waturejeshee fedha zetu,” alisema Badru.

Aidha, alisema nia ya kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao ni kuutangazia na kuutarifu umma juu ya watu wanaokwamisha wanafunzi wengine kukosa fursa ya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa kuwa fedha iliyopo bado haitoshelezi.

Alisema bodi hiyo ilitoa muda wa wiki nne kwa wadaiwa hao sugu na baadaye kuwaongezea tena muda wa wiki mbili, unaoishia Desemba 30, mwaka huu, hivyo kinachofuata ni utekelezaji kwa wale walioshindwa kuitumia fursa hiyo ya kujisalimisha.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya muda huo kwisha na bodi hiyo kuanza kuchapisha majina na picha za wadaiwa hao, wale watakaopatikana kwa kushindwa kulipa madeni yao, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipia gharama za usumbufu wa kuwatafuta.

Alisema utaratibu wa kukopesha ni mfumo unaowezesha wanafunzi wengi zaidi, kupata fursa ya kuendelea na masomo yao ya elimu ya juu, hivyo ni vyema wanafunzi wote wanaopata fursa ya kukopa wahakikishe wanalipa kwa muda muafaka uliowekwa kisheria.

Badru alisema kwa mujibu wa marekebisho ya sheria hiyo ya Bodi ya Mikopo, imewaongezea muda wa kuanza kulipa wanafunzi walionufaika na mikopo kutoka miezi sita hadi miaka miwili ili kutoa fursa ya kujipanga na kutafuta ajira.

Aidha, alibainisha kuwa sheria hiyo pia imeongeza kiwango cha makato kwa waajiriwa walionufaika na mikopo ya HESLB kutoka asilimia nane ya mishahara yao hadi asilimia 15.

“Tunawashukuru sana wadau kwa kuwezesha kutoa maoni yao yenye tija kwenye sheria hii katika eneo hili sisi tulipendekeza kiwango cha makato kifikie hadi asilimia 30 na zaidi, lakini kupitia maoni mbalimbali ya wadau wakiwemo wa wabunge walipendekeza kiwango kiwe asilimia 15 tu,” alisema.

Alisema ili kuweza kutimiza lengo la kuhakikisha kila mnufaika na mikopo hiyo aliyeajiriwa analipa deni lake, pamoja na kuwabana wadaiwa, bodi hiyo imeanza mkakati wa kuwabana waajiri wasiotimiza wajibu wao kisheria kupitia marekebisho hayo ya sheria.

“Tumeunda kikosi kazi kinachojumuisha timu ya wataalamu kutoka sehemu mbalimbali nyeti, kitakachoanza kufanya kazi kuanzia Januari 2, mwaka huu, ya kuhakiki kila ofisi ya waajiri sugu ili kubaini kama ama wamewasilisha majina ya wanufaika wa mikopo hii au wanawakata bila kuwasilisha michango hiyo kwa bodi,” alisema.

Alisema waajiri watakaobainika kwenda kinyume na sheria hiyo kwa kutoisaidia bodi kupata waajiriwa wanaodaiwa au kutowasilisha makato yao, wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa kulipa faini isiyopungua makato hayo waliyoshindwa kuyawasilisha na endapo watashindwa watakabiliwa na adhabu ya kifungo cha muda wa miezi 36 jela.

“Lakini pia sheria hii imewawajibisha wale waliokopa kuhakikisha wanapeleka wenyewe taarifa zao kwa bodi ili waweze kuwekewa utaratibu wa makato, yeyote atakayebainika kutowasilisha taarifa zake naye atawajibishwa,” alisisitiza.

Halikadhalika, Badru alisema marekebisho hayo ya sheria, pia yamegusa wanufaika wa mikopo hiyo ya elimu ya juu, ambao hawako kwenye mfumo rasmi wa ajira, ambao nao wanatakiwa kurejesha kiasi kisichopungua Sh 100,000 kila mwezi.

Akizungumzia mafanikio tangu bodi hiyo itoe muda wa hiari kwa wadaiwa sugu kulipa wenyewe madeni yao, Mkurugenzi huyo alisema makusanyo ya fedha, yameongezeka kutoka Sh bilioni mbili mpaka nne kwa mwezi hadi Sh bilioni nane.

Alisema tangu muda huo utolewe jumla ya wanufaika 42,700 wamejitokeza wenyewe kwa hiari na kulipa madeni yao huku wengine wakilipa deni lote na wengine wakiyapunguza.

Hadi sasa bodi hiyo ya mikopo ina jumla ya Sh bilioni 300 zilizoiva, inazozidai kwa wadaiwa hao sugu na kati ya fedha hizo ni Sh bilioni 140 pekee ndio zimelipwa.

Kwa mujibu wa HESLB kuanzia Juni, mwaka huu, jumla ya wanafunzi 379,179 wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na bodi hiyo tangu ianzishwe Juni, mwaka 1994 na jumla ya Sh trilioni 2.6 zimeshatolewa kwa wanafunzi hao.

Jumla ya wahitimu wa elimu ya juu wa zamani 238,430 walionufaika na mikopo ya HESLB, wanatakiwa kuanza kulipa madeni yao, ambayo ni kiasi cha Sh trilioni 1.4, baada ya muda waliotakiwa kulipa kwa mujibu wa sheria kuisha.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com