Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM KUANZA KUTUMBUANA KUSAFISHA CHAMA...MATAJIRI WA HILA NDANI YA CCM KUFUKUZWA


Mabadiliko yaliyofanywa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yamekuja na mkakati mpya wa kuwavua ‘gamba’ makada wa chama hicho wenye ukwasi waliovuna kinyume na taratibu.


Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema kuwa wako katika mkakati wa kukisafisha zaidi chama hicho, akiwataka matajiri wenye ‘makandokando’ wajiondoe mapema.


“Kuwa tajiri si dhambi na si kwamba CCM inafukuza matajiri, hapana. Tatizo letu kama CCM katika mwelekeo mpya, mtazamo mpya na maegeuzi yanayofanyika, hatuhitaji kuwa na aina ya matariji wanaojipatia utajiri wao kwa hila, kwa rushwa na kwa dhuluma,” alisema Polepole katika mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini.


“Ukijiona wewe ni tajiri na mikono yako ni michafu kwa maana ya kuwa na makando ya kukosa uaminifu, hulipi kodi, ukae mbali na CCM,”aliongeza.


Alisema watawachukulia hatua za kuwaondoa ndani ya chama hicho na kuwakabidhi kwa vyombo vya dola ili wachukuliwe hatua za kisheria.


Tangu alipochaguliwa, Polepole amekuwa akisisitiza kuwa chama hicho kitajikita katika msingi wake wa kuwatumikia wanyonge.


Mkakati huo wa kuwang’oa matajiri wasiowaaminifu ndani ya chama hicho unafanana na oparesheni iliyobatizwa jina la ‘Vua Gamba’ ndani ya chama hicho miaka kadhaa iliyopita, iliyolenga kuwang’oa viongozi na vigogo ambao walibainishwa kujipatia mali kinyume cha utaratibu na mafisadi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com