Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mbali
na jitihada za makusudi za Serikali na wadau wa mapambano dhidi ya
UKIMWI nchini bado hali siyo ya kuridhisha ambapo Jiji la Dar es Salaam
linashika nafasi ya Sita barani Afrika kwa maambukizi ya ugonjwa huo.
Dar
es Salaam ambalo ni Jiji kubwa kuliko yote Tanzania linakadiriwa kuwa
na watu 210,000 wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambapo kati yao asilimia
58 ni wanawake, na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012
idadi ya wakazi wa jiji hilo inakadiriwa kuwa Milioni 5.
Kwa
mujibu wa taarifa ya hali ya UKIMWI duniani kutoka Shirika la Mpango wa
UKIMWI la Umoja wa Mataifa - Tanzania (UNAIDS) kwa mwaka 2015, Jiji la
Dar es Salaam limekuwa kati ya majiji Barani Afrika yenye kiwango
kikubwa cha maambukizi ya UKIMWI.
Afisa
wa UNAIDS Tanzania, Fredrick Macha anasema asilimia 16 ya maambukizi
yote mapya Tanzania Bara yanatokea katika jiji la Dar es Salaam ambapo
kwa wanawake wenye umri mdogo wa miaka 15-24 kiwango cha maambukizi
kimefikia asilimia 7%,sababu kubwa ikiwa ni kujiingiza katika ngono
wakiwa na umri mdogo pamoja na biashara ya ukahaba.
Anafafanua
kuwa maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto Jijini Dar es Salaam
ni asilimia sita (6%) licha ya jitihada kubwa za Serikali na wadau
mbalimbali wa mapambano dhidi ya UKIMWI,kuelimisha na kuhamasisha
wajawazito kupima na kufuata ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kujikinga
na VVU.
“Takwimu
za Wizara ya afya za mwaka (2011-2012), mtu mmoja kati ya watu watano
jijini Dar es Salaamana mahusiano ya kimapenzi na zaidi ya mtu mmoja,na
mara nyingi wanafanya ngono zisizo salama hivyo hicho ni kiashiria
kikubwa cha ongezeko la maambukizi hasa kwa wana ndoa”alisema Macha.
Aidha
amevitaja baadhi ya vichocheo na viashiria vinavyochangia uwepo wa
ongezeko kubwa la maambukizi katika jiji hilo kuwa ni ukuaji wa kasi wa
shughuli za kiuchumi na kibiashara unaosababisha muingiliano wa watu
kutoka Mikoa mbali mbali nchini pamoja na mataifa mengine.
Dar
es Salaam kama yalivyo majiji mengine duniani yenye muingiliano wa
tamaduni na desturi mbalimbali limeathirika pia na makundi yanayoelezwa
kuchochea maambukizi mapya ya UKIMWI kama vile wafanya biashara ya
ngono, wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na watumiaji wa madawa ya
kulevya na kwa kujidunga.
“Kwa
mujibu wa takwimu hizo, kati ya wanawake 4 wanaojihusisha na biashara
ya ngono, mmoja ni mwaathirika na virusi vya UKIMWI (sawa na asilimia
26).Vile vile kati ya watu watano wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja,
mtu mmoja ameathirika, sawa na asilimia 22.3) na kati ya watu sita
wanaotumia madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano, mmoja ni
mwathirika wa virusi vya UKIMWI (sawa na asilimia 15.5),”alisema Macha.
Aidha
Macha alisema pamoja na changamoto mbalimbali, Jiji la Dar es Salaam
limependekezwa kuwa moja ya majiji machache ya mfano ulimwenguni katika
mkakati wa dunia wa kuimarisha udhibiti wa UKIMWI kwenye majiji (UNAIDS
Fast Track Cities Initiative).
Mkakati
huo ni kuyafanya majiji makubwa Afrika kuwajibika zaidi katika kuongeza
ufanisi kwenye mapambano dhidi ya UKIMWI katika maeneo ya mijini kwani
kasi ya maambukizi na wingi wa maambukizi yapo mijini.
Pamoja
na majiji kuwa na rasilimali nyingi, mifumo ya utoaji huduma za afya
bado inaandamwa na changamoto mbalimbali, hususani katika kuandaa na
kutekeleza mipango mizuri yenye kuhakikisha ushirikishwaji wa watu wote
hasa makundi maalumu katika jamii, ambayo kiwango cha maambukizi ni
kikubwa.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira
na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama anasema takwimu zilizopo sasa
zinaonyesha kuwa asilimia 6.2 ya wanawake nchini wameambukizwa ugonjwa
wa ukimwi ikilinganisha na asilimia 3.8 ya wanaume,jambo ambalo
linahitaji jitihada zaidi kujikinga.
“Kwa
mujibu wa Utafiti wa Viashiria vya Virusi vya UKIMWI (VVU) na Maralia
(THMIS) wa mwaka 2011/2012 kwa upande wa Tanzania Bara vinaonyesha kuwa
idadi kubwa ya wanawake wameambukizwa ugonjwa huo kuliko wanaume.
Waziri
Mhagama anasema kuwa kutokana na utafiti huo, maambukizi ya virusi vya
UKIMWI kwa upande wa Tanzania Bara ni asilimia 5.3 na inakadiriwa kuwa
jumla ya watanzania 1,538,382 wanaishi na VVU ambapo vijana wenye umri
kati ya 15-24 ni asilimia 10.6 na watoto walio chini ya miaka 15 ni
11.8.
Aliongeza
kuwa UKIMWI bado ni janga kubwa nchini Tanzania kwani takwimu
zinaonyesha kuwa maambukizi mapya yanakadiriwa kufikia watu 48,000 kwa
mwaka hali ambayo inaashiria kupoteza nguvu kazi kubwa katika nchi
yetu hivyo Tanzania itendelea kushirikiana na nchi nyingine
Duniani,pamoja na mashirika ya kupambana na UKIMWI kuhakikisha janga
hilo linatokomezwa ifikapo mwaka 2030.
Alisema
Serikali inaendelea kuwahamisha wananchi waendelee kujitokeza kupima
afya zao kwa hiari ili wajitambue na kujua namna ya kujilinda kwani
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasisitiza nchi wanachama kuwaanzishia
dawa mara moja watu wote watakaopima na kugundulika kuwa na VVU,bila
kusubiri hadi kinga zao zipungue.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dr.
Leonard Maboko alisema kuwa kwa mwaka 2015 walioambukizwa VVU walikuwa
Watanzania 2,100,000 ambayo ni idadi kubwa ukilinganisha na idadi ya
sasa lakini pamoja na kushuka kwa idadi hiyo wananchi wanatakiwa
kuendelea kujilinda mara dufu.
”Ingawa
maambukizi ya VVU yameshuka kutoka Watanzania 2,100,000 hadi 1,538,382,
Watanzania hatutakiwi kubweteka bali tunatakiwa tufanye jitihada za
pamoja kuhakikisha janga hili linafikia mwisho,”alisema Dr. Maboko.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu alisema
wataalam wa afya wametuambia UKIMWI unapungua nchini Tanzania, suala
hilo linatokana na misaada mbalimbali tunayoipata kutoka nchi wahisani
kwahiyo ili kutokomeza kabisa suala la upungufu wa dawa na misaada kwa
waathirika wa ugonjwa huo Watanzania wanahitaji kujichangia wenyewe na
sio kutegemea fedha za wahisani peke yake.
Alifafanua
kuwa ili kuwezesha suala hilo,Sheria Na. 5 ya mwaka 2015 imeitaka
Wizara yenye dhamana kuwa na Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI pamoja na Bodi
yake hivyo, kuanzishwa kwa Mfuko huo kutaleta chachu kwa Watanzania
kuungana kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI (VVU) pamoja na
kuwahudumia wananchi wanaoishi na virusi hivyo.
“Kwa
kawaida fedha zinazotoka kwa wahisani huwa zina mwisho wake hivyo
Tanzania tunazindua Bodi rasmi itakayosimamia Mfuko huo ili na sisi
tuongeze nguvu pale wahisani watakapoishia,”alisema Mama Samia.
Naye
muathirika wa UKIMWI, (jina limehifadhiwa) ameishkuru Serikali kwa
kuwasaidia kwa hali na mali watu wenye ugonjwa huo kwani sio wote wenye
ugonjwa huo wameupata kwa kujitakia.
“Kitendo
hiki kinatufanya tusijione wanyonge wala kukata tamaa kwani Serikali
yetu haitutengi inatupa ushirikiano sawa na watu wengine wasio na
maambukizi ya ugonjwa huu,”alisema muathirika huyo.
Tarehe
1 Disemba kila mwaka ni siku maalumu ambayo tunaadhimisha Siku ya
UKIMWI duniani, siku ambayo kwa pamoja tunaungana na watu wote
wanaokadiriwa kufikia milioni 78 ambao tayari wameshapata mambukizi na
watu milioni 35 ambao tayari wamefariki ulimwenguni kote kutokana na
athari zitokanazo na maambukizi ya UKIMWI.
Social Plugin