Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

GARI LAUA WATU WANNE WAKIWEMO POLISI WAWILI NA KUJERUHI 9 DODOMA

Watu wanne wakiwamo polisi wawili, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupindua katika kijiji cha Seruka kata ya Chipogoro tarafa ya Rudi wilayani Mpwapwa mkoa wa Dodoma.


Ajali hiyo ilitokea Desemba 19, mwaka huu, saa 11:30 jioni katika kijiji hicho baada ya gari walilokuwa wakisafiria T517 CDL Toyota Alphat katika barabara kuu ya Dodoma- Iringa, kuacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi tisa.


Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ernest Kimola, amesema gari hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na Aggrey Lucas, baada ya kufika katika kijiji hicho, liliacha njia na kupinduka na kusababisha vifo vya askari Konstebo Mahende na Konstebo Sasi Mwita ambaye ni askari mkoa wa Songwe.


Kamanda Kimola amewataja wengine waliofariki katika ajali hiyo ni mke wa Konstebo Mwita, Pendo Mwita na Emaculata Nyangi.


Amewataja majeruhi wa ajali hiyo ni Neema Mwita (8), Jenifa Mwita (4), Nyangi Wambura (23), Konstebo Nashon (23) ambaye ni polisi kituo cha Tunduma na Baraka Chacha (9).


Wengine ni Juli Mwita (6), Pc Enock ambaye ni mmiliki wa gari lililopata ajali, Makongoro Charles na Elizabeth Cosmas ambao wote wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Dodoma.


Aidha, kamanda Kimola amesema miili ya marehemu hao waliofariki katika ajali hiyo, imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa wa Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com