JAJI Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ndiye atakayesikiliza rufaa ya kutaka dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Desemba 28 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga alisema rufaa hiyo namba 126 ya mwaka 2016, imepangiwa kusikilizwa na Jaji huyo. Alisema kimsingi wanalalamikia uamuzi wa Mahakama kutomwachia huru, licha ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kumpatia dhamana.
Awali, uamuzi uliotolewa Novemba 11 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha na Hakimu Desderi Kamugisha, ambapo Lema anakabiliwa na kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli, uliweka wazi dhamana.
Hakimu Kamugisha alikubali kutoa dhamana kwa madai kuwa sheria haizuii kumpa dhamana mtu kwa kesi ya uchochezi, ila kabla ya kutoa masharti ya dhamana licha ya kutamka dhamana ipo wazi, mawakili wa serikali walipinga kumpatia dhamana Lema, kwa madai wameonesha nia ya kukata rufaa.
Kutokana na mawakili hao kusema hivyo, Hakimu aliamua kesi hiyo ibaki kama ilivyo na mtuhumiwa asubiri maamuzi ya Mahakama Kuu.
Lema alilazimika kwenda mahabusu hadi sasa katika Gereza Kuu la Kisongo. Baada ya hatua hiyo, mawakili wa Lema wakiongozwa na Sheck Mfinanga, walianza kutafuta suluhisho la mteja wao kupata dhamana na walianza na kuandika maombi na kuitaka Mahakama Kuu kufanya marejeo kwa kuitisha faili la kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Lakini, ombi lilitupwa na Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi, Novemba 11 mwaka huu kwa madai kuwa walikosea, badala ya kufanya marejeo walitakiwa kukata rufaa. Mawakili hao walilazimika kukata rufaa siku hiyo hiyo na Desemba 2 mwaka huu, ilitupwa na Jaji Fatuma Masengi kwa madai kuwa ilikuwa nje ya muda.
Baada ya hatua hiyo, mawakili hao walipeleka ombi Mahakama Kuu, kuomba kuongezewa muda wa kupeleka notisi ya kukata rufaa yao juu ya dhamana na hatimaye Desemba 20, Jaji Dk Modesta Opiyo, alikubali na kumwongezea muda Lema wa siku 10.
Siku hiyo ya kuongezewa muda, mawakili wa Lema walifanikiwa kukata rufaa hiyo. Lema anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi katika mahabusu ya Gereza Kuu Kisongo.
Alikamatwa Novemba 2 mwaka huu nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na alifikishwa mahakamani Novemba nane mwaka huu, akikabiliwa na mashitaka ya uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli.