Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI POLISI WALIVYOVAMIA OFISI ZA JAMII FORUMS NA KUFANYA UPEKUZI NA KUONDOKA NA VIFAA VYA OFISI




Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Maxence Melo.
*****
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limevamia ofisi za mtandao wa Jamii Forums (JF) na kufanya upekuzi na kuondoka na vifaa zikiwamo kompyuta mpakato (laptop).

Askari hao walivamia ofisi hizo jana mchana wakiwa wamefuatana  na Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Maxence Melo, wakafanya upekuzi na kuwahoji baadhi ya wafanyakazi.

Baada ya kufanya upekuzi ndani ya ofisi hiyo walielekea nyumbani kwa mkurugenzi huyo, kufanya upekuzi kabla ya kumrudisha rumande kwa vile hakufikishwa mahakamani.

MTANZANIA lilimtafuta Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kwa simu ili kupata taarifa kwa kina, lakini haikuweza kupokewa.

Juzi, akizungumza na MTANZANIA, mwanaharakati wa kutetea Uhuru wa Mawasiliano, Simon Mkina, alisema Melo alikamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi ambako aliwekwa selo.

Alisema Melo anakabiliwa na mashtaka ya kuzuia upelelezi wa makosa ya mtandao kwa kushindwa kutoa taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wa Jamii Forums ambazo polisi walizihitaji.

“Max (Melo)alifika kituoni hapo kuitika wito wa polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lakini alipofika Kituo Kikuu cha Polisi alinyimwa dhamana kwa madai ya kuwapo amri kutoka kwa wakubwa,” alisema Mkina akimkariri mmoja wa maofisa wa polisi.

Mkina alisema hata baada ya kuwasiliana na mwanasheria wa Melo, Nakazeel Tenga na kushughulikia dhamana yake, ilishindikana kwa maelezo kuwa alipaswa kulala kituoni hapo hadi jana.
Na HERIETH FAUSTINE-MTANZANIA DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com