KIJANA AFUNGWA JELA MAISHA KWA WIZI WA SIMU AINA YA TECNO

Kesi ya wizi wa simu aina ya Tecno iliyochukua takriban miaka miwili mahakamani, imefika tamati kwa mtuhumiwa kufungwa maisha jela. 


Hukumu hiyo ilifikiwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, baada ya mtuhumiwa Kassim Salum (18) kukutwa na hatia kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia nguvu wa simu yenye thamani ya Sh110,000. 


Mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Januari 28, mwaka jana katika Mtaa wa Ghana Magenge eneo la Buguruni jijini Dar es Salaam. 


Ushahidi uliotolewa na mashahidi watano uliiwezesha mahakama kukubaliana na madai ya mlalamikaji Lutifia Mohamed. 


Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Flora Haule alisema, “Baada ya kusikiliza mashahidi wote watano wa upande wa jamhuri, mahakama inaona wamethibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa.” 


Akipitia ushahidi huo, hakimu Haule alisema mshtakiwa alimsukuma mlalamikaji na kuangukia katika karai la mafuta ambalo lilikuwa jikoni. 


Mashahidi hao waliieleza jinsi mshtakiwa alivyomvamia mlalamikaji akimtaka atoe simu aliyokuwa nayo na katika purukushani hizo, alimpiga ngumi tumboni hali iliyosababisha kuishiwa nguvu. 


Ilielezwa kuwa kutokana na kupigwa, mlalamikaji aliirusha simu upande wa pili ambapo kulikuwa na muuza chipsi, hivyo Salum aliamua kumuachia mlalamikaji ili aende kuifuata. 


Hata hivyo, wakati mlalamikaji anajaribu kuokota simu yake, Salum alimsukuma akaangukia katika karai la mafuta ya moto na kumsababishia kuungua eneo lote la mgongoni. Inadaiwa baada ya hapo Salum alichukua simu hiyo na kutoweka nayo. 


Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto aliomba mahakama impe adhabu kali Salum ili aweze kujifunza kwa kuwa amemtia mlalamikaji ulemavu wa kudumu. 

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea na Salum aliomba isimpe adhabu kali akisema si yeye aliyechukua simu hiyo, bali ni chuki binafsi za mitaani wanakoishi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post