Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KINGUNGE : BILA TUME HURU YA UCHAGUZI NA KATIBA MPYA,VYAMA VYA UPINZANI VISAHAU KUSHINDA URAIS

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amesema bila ya kuwa na tume huru ya uchaguzi na Katiba Mpya, vyama vya upinzani visahau kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.


Kauli ya Kingunge imekuja siku moja baada Rais John Magufuli kumteua Jaji Themistocles Kaijage kuwa mwenyekiti mpya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) baada ya Jaji Damian Lubuva kufikia muda wake wa kustaafu.


Kwa muda mrefu, NEC imekuwa ikilalamikiwa na vyama vya upinzani kwa kutokuwa huru kwa sababu ya uongozi wake wote huteuliwa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, huku sheria zikikataza matokeo ya nafasi ya urais kupingwa mahakamani.


Mbali na mwenyekiti kuteuliwa na Rais, wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo ni wakurugenzi wa wilaya ambao pia huteuliwa na Rais kwa kuwa NEC haina wafanyakazi wake kote nchini.


Akizungumza katika mkutano wa kuwafariji vijana waliokamatwa na Jeshi la Polisi na kushtakiwa kwa makosa yaliyohusu Uchaguzi Mkuu uliopita, uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Kingunge aliwatia moyo vijana hao, akisema hakuna ushindi unaopatikana bila kupambana.


Kingunge, aliyetumia muda mrefu kueleza historia ya maisha yake katika siasa na jinsi alivyopambana katika harakati za kudai uhuru, alisema hali ya sasa ni mbaya kuliko wakati wa wakoloni wa Kiingereza ambao walikujwa wakali, kwa sababu CCM haifuati Katiba wala sheria.


“Yako mambo ambayo itabidi tujitahidi yaamuliwe sasa kabla ya 2020. Mambo hayo makubwa kwanza ni tume huru (ya uchaguzi). Suala hilo lazima lizungumzwe sasa, hatuwezi kwenda 2020 na tume ya sasa na Katiba ya mwaka 1977. Tukienda hivyo sahau habari ya upinzani kushinda uchaguzi,” alisema.


Kingunge ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya waziri anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na mkuu wa mkoa alisema, “(Pia) Sheria inayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais kuhojiwa. Hivi sasa sheria inasema matokeo ya uchaguzi wa Rais hayahojiwi mahakamani. Lazima hilo suala lipate jibu sasa. Kwa hiyo Katiba na sheria iseme, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kuhojiwa mahakamani. Tusipokuwa na hilo, tutakuwa na matatizo makubwa sana.”


Alisema pamoja na kwamba Chadema inapendwa na wananchi wengi na Edward Lowasa aliyegombea urais kwa tiketi chama hicho, anapendwa, bado ni vigumu kushinda kwa sababu mfumo uliopo sasa.


“Tufanye yoyote, lakini tuhakikishe, ama tunapata Katiba Mpya au vipengele hivi vya sheria vinafanyiwa marekebisho. Kwa maoni yangu, kundi hili lililo madarakani bila shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, halitataka mabadiliko,” alisema.


Alisema enzi zao walifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitolea kwa nguvu na wengine, na yeye akiwamo, waliacha kazi za mishahara mikubwa na kujiunga na Tanu kupigania uhuru.


“Tulifanikiwa kupata uhuru kwa sababu walijitoa mhanga. Wengi tu waliacha kazi, mtu anamaliza chuo kikuu anasema sitaki kazi anaingia Tanu kusaidia. Kwa hiyo tukawa na jeshi kubwa la vijana waliohakikisha nchi inapata uhuru,” alisema.


“Ninyi mnapambana katika mazingira magumu na wazee wenzenu walipambana katika mazingira hayo. Haikuwa rahisi. Wapo wengi walitusaliti, wengine hawakufanya lolote. Baba yangu tuligombana, nilipoacha kazi kwenda kuitumikia Tanu. Miezi sita hatukuzungumza.”


Akizungumza mkutano huo, Lowassa, ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwatia moyo vijana walioshtakiwa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, akisema bado jeshi kubwa la vijana linahitajika.


“Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Si haki kusema unakwenda mahali pengine, mwenzako amepasafisha, safisha pa kwako. Nimefurahia moyo huo. Kama alivyosema Ngombale, tunataka jeshi kubwa zaidi, watu wengi zaidi,” alisema Lowassa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com