MADEREVA wa bodaboda wametajwa kuongoza kufanya matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Pwani yanayohusisha ubakaji, ulawiti na kuwapa mimba wanafunzi.
Imeelezwa kuwa, kati ya watuhumiwa 10 wa makosa hayo ya ukatili, watatu ni madereva wa bodaboda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonaventura Mushongi, alisema hayo alipokuwa akizungumza na madereva wa bodaboda na wananchi na kusema kuwa hilo ni janga ambalo linapaswa kupigiwa kelele na jamii yote.
Alisema matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Pwani yameongezeka kutoka 257 kwa kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka jana na kufikia 310 kipindi kama hicho mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la makosa 53.
Aidha imebainika kuwa madereva wa bodaboda wanaongoza kwa kufanya matukio hayo ya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti, kuwapa mimba wanafunzi.
Kamanda Mushongi alisema utafiti uliofanywa na dawati la jinsia na watoto mkoani hapo, limebaini kwamba baadhi ya madereva bodaboda hujihusisha na vitendo hivyo jambo ambalo linapaswa kupigwa vita.
“Madereva hao wasaidiane kuwafichua wale ambao wamekuwa wakiitia doa kazi hiyo na kuwachafua mbele ya uso wa jamii na kuanzisha timu za ulinzi na usalama ili kupeana elimu na kutoa taarifa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia,” alisema.
Alisema kupitia umoja wao wapinge matendo yote ya ukatili na udhalilishaji na kuwalinda watoto ili kupambana dhidi ya vitendo vya ukatili kwa lengo la kupunguza na kutokomeza vitendo hivyo.
Hata hivyo, Mushongi aliwaomba wazazi kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto kwa karibu, badala ya kuwaachia kina mama pekee ambao baadhi yao huwaachia wasichana wa kazi jukumu hilo.
Alibainisha suala hilo la wazazi kuwa mbali husababisha baadhi ya watoto kujitumbukiza katika vitendo vya ngono wakiwa katika umri mdogo na kusababisha kupata ujauzito, ama kuambukizwa magonjwa ikiwemo virusi vya Ukimwi.
Via>>Habarileo
Social Plugin