Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKE WA ALIYETOBOLEWA MACHO NA SCORPION AELEZA MAHAKAMANI JINSI MMEWE ALIVYOCHOMWA VISU

Stara Sudi, mke wa Saidi Mrisho ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala, jinsi alivyoshtuka baada ya kupokea simu aliyopiga mumewe kuwa amevamiwa na kuchomwa visu machoni, mgongoni na tumboni. 

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa Salum Njwete (34) maarufu ‘Scropion’, Stara alimueleza Hakimu Mkazi, Flora Haule kuwa Septemba 6, saa tano usiku akiwa amelala alipokea simu yenye sauti ya mumewe ikieleza kuwa amevamiwa. 

“Aliniambia mama Nancy nimechomwa visu hata kuona sioni hapa nilipo nipo Buguruni,” alidai Stara ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa mashtaka. 

Alidai tangu wafunge ndoa na mumewe Oktoba 2015 , Said alikuwa akifanya kazi ya kinyozi katika saluni ya Rodgers iliyopo Tabata Sanene. 

“Baada ya kuongea na mume wangu, simu ilikatika lakini wakati natafuta nguo nivae simu ileile ilipiga na nilipopokea sauti ya mtu mwingine iliongea ambaye ndiye mwenye simu na aliniambia kuwa mume wangu ana hali mbaya hivyo nifanye haraka niende Hospitali ya Amana,” alidai Stara. 

Baada ya kupata taarifa hizo, alidai alimweleza mtoto wao mkubwa, Abdul Said (12) kuwa anaelekea Amana. Lakini kabla ya kwenda huko alichukua pikipiki na kwenda Mabibo Hosteli anakoishi mama mkwe wake kumweleza taarifa hiyo na kwamba waliambatana hadi Amana. 

Alidai wakiwa njiani, walimjulisha mdogo wa Saidi, Yahaya Kisukari (23) kuwa kaka yako amepata matatizo ya kuvamiwa na mtu akachomwa visu na yupo Hospitali ya Amana. 

“Tulipofika Amana, tuliruhusiwa kuingia wodini na kumuona mume wangu akiwa amefungwa bandeji machoni na sehemu nyingine za mwili, huku damu ikivuja sehemu mbalimbali za mwili. Hata nguo aliyovaa ilikuwa imejaa damu,” aliiambia Mahakama na kuongeza:“Baada ya kumvua nguo zilizo- kuwa zimetapakaa damu, tulipewa rufaa kwenda Muhimbili kwa ajili ya matibabu na wakati huo ilikuwa imeshafika saa sita usiku.” 

Stara alidai baada ya kumuona mumewe aliyechomwa visu na mtu aliyemtaja kwa jina la Scorpion, alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Buguruni. 

“Baada ya kutoa maelezo Polisi Buguruni na askari kwenda kuchukua maelezo ya mume wangu Muhimbili, tulikwenda kumkamata mshtakiwa Salum Njwete,” alidai. 

Alidai: “Septemba 8, tulirudi tena Muhimbili na kupewa taarifa na daktari wa macho aliyemfanyia upasuaji Said kuwa macho yake hayataona tena.” Stara alidai tangu waoane na mumewe, hajawahi kupata malalamiko yoyote kuwa mwenza wake huyo ni mwizi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com