MSAJILI MKUU WA MAHAKAMA TANZANIA AWATAKA MAHAKIMU KUZINGATIA SHERIA

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Katrina Revocati amewataka mahakimu nchini kuzingatia sheria katika utendaji wao wa kazi hasa katika utoaji wa dhamana. 


Kauli ya Msajili imekuja wakati kukiwa na malalamiko dhidi ya baadhi ya mahakimu kuwanyima dhamana washtakiwa ilhali mashtaka yao yanaruhusu. 


Aidha, kauli ya msajili huyo mkuu imekuja wakati mawakili wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wakipambana ili mteja wao apate dhamana baada ya kukwaa kisiki katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. 


Mashtaka ambayo kwa mujibu wa sheria dhamana zake zimezuiwa ni ya mauaji ya kukusudia, uhaini, utakatishaji wa fedha, wizi wa kutumia silaha, usafirishaji binadamu na dawa za kulevya. 


Hata hivyo, Mahakama inaweza kuzuia dhamana endapo kutakuwa na pingamizi la kisheria, na mara nyingi mapingamizi hayo yamekuwa yakiambatana na hati kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). 


Msajili huyo alitoa maagizo hayo jana mjini Moshi alipokuwa akizungumza na mahakimu wa ngazi zote katika mahakama za mjini Moshi baada ya kumaliza ziara ya kikazi katika mkoa wa Kilimanjaro. 


Taarifa iliyotolewa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bernard Mpepo ilisema msajili huyo waliwataka mahakimu watunze maadili yao ili kujenga imani kwa jamii. 


Msajili mkuu pia alitembelea Gereza Kuu la Karanga mjini Moshi na kufanya ukaguzi wa kawaida na kisha kuzungumza na wafungwa, mahabusi na wafanyakazi wa gereza. 


Akiwa katika gereza hilo, msajili mkuu alisema mkakati wa Mahakama ni kuona wateja wanapata huduma bora na ya haraka na tayari mahakimu wamepewa malengo ya kumaliza kesi haraka. 


Ili kuboresha huduma, alisema mwaka 2017 wamekubaliana katika mahakama ya mwanzo, shauri lolote lisikae zaidi ya miezi sita wakati mahakama ya wilaya na mkoa shauri lisikae zaidi ya miezi 12. 


Pia mahakama imeingia mkataba na Shirika la Posta kusambaza nakala za hukumu kwa wateja na nakala ya hukumu itakuwa inamfikia mdau ndani ya siku 21. 


Chini ya mkakati huo, nakala ya mwenendo wa shauri utamfikia mteja wa mahakama ndani ya siku 21.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post