POLISI MBEYA WAPAMBANA NA MAJAMBAZI,WAUA MAJAMBAZI WAWILI
Wednesday, December 21, 2016
Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya wamefanikiwa kuzuia tukio la ujambazi katika mapambano ya kurushiana risasi na watu waliosadikiwa kuwa ni majambazi na kuua wawili kati yao.
Taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Dhahiri Kidavashari imesema kuwa mnamo tarehe 19.12.2016 majira ya saa 1:45 jioni katika Kijiji cha Busisya, Wilaya ya Rungwe, Askari Polisi walipata taarifa za siri za kuwepo kwa majambazi wenye silaha ambao walikuwa na lengo la kufanya uvamizi katika Duka la Mfanyabiashara wa soda na bia za jumla ambaye pia ni wakala wa kutuma na kupokea pesa kwa njia ya mtandao.
Askari hao walianza kuwafuatilia majambazi hao na muda wa saa 1:45 jioni askari walikutana na majambazi hao wakiwa wamepakiana katika pikipiki ambapo baada ya majambazi hao kugundua kuwa wanafuatiliwa na askari walianza kuwarushia risasi askari na ndipo yalitokea majibizano ya risasi kati ya askari na majambazi hao.
Askari walifanikiwa kuwapiga risasi majambazi wawili ambao walifariki papo hapo na mmoja wao aliweza kutupa silaha aliyokuwa akiitumia na kukimbia.
Aidha katika tukio hilo silaha bunduki tatu pamoja na risasi tisa ziliweza kupatikana zilizokuwa zinatumiwa na majambazi hayo. Silaha hizo ni Mark IV yenye namba 38482 na risasi mbili, Short Gun Greener yenye namba G.73878 na risasi 01 na Gobole lililotengenezwa kienyeji ambalo halina namba na risasi 06.
Pia baada ya kupekuliwa majambazi hao walikutwa na vitu vingine ambavyo ni Rungu moja, Praizi moja, Bisibisi moja, mafuta ya cherehani, koti la ngozi rangi ya brown pamoja na begi dogo rangi nyeusi ambalo lilitumika kuhifadhi vitu hivyo.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Serikali Makandana Wilaya ya Rungwe kwa uchunguzi wa kitabibu na bado haijatambulika. Msako unaendelea. Katika tukio hilo hakuna mali iliyoporwa wala askari kupata madhara. Jitihada za kumtafuta jambazi aliyekimbia zinaendelea, Upelelezi unaendelea.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin