Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AWAAPISHA VIONGOZI WA TUME YA UCHAGUZI,MAJAJI WA MAHAKAMA YA RUFANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 23 Desemba, 2016 amewaapisha viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Majaji wa Mahakama ya Rufani aliowateua jana tarehe 22 Desemba, 2016.

Hafla ya kuwaapisha viongozi hao imehudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Mhe. Anjellah Kairuki, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Mcheche Masaju na Viongozi wengine mbalimbali.

Walioapishwa ni Mhe. Mhe. Jaji Semistocles Simon Kaijage aliyeapishwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid aliyeapishwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jaji Harold Reginald Nsekela aliyeapishwa kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Viongozi hawa watashika nyadhifa hizo kwa kipindi cha miaka mitano.

Kwa upande wa Majaji walioapishwa kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni Mhe. Jaji Rehema Kiwanga Mkuye, Mhe. Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi na Mhe. Jaji Dkt. Gerald Alex Mbonimpa Ndika, Mhe. Jaji Jackobs Casthom Mwatebela Mwambegele.

Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki hapa nchini Mhe. Yesamin Eralp ambapo viongozi hao wamezungumzia uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki hususani katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli wamemtembelea na kumpa pole Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kufuatia kifo cha Dada yake aitwaye Efrazia Pengo aliyefariki dunia jana tarehe 22 Desemba, 2016 katika Kijiji cha Mwazye, Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa akiwa na umri wa miaka 79.

Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Mama Janeth Magufuli wamemtembelea Kardinali Pengo katika makazi yake yaliyopo Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
23 Desemba, 2016.
Mhe. Jaji Semistocles Kaijage akisaini hati ya kiapo mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kiapo cha kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Jaji Mstaafu Hamid Mohamed Hamid kuwa Makamu kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapishaJaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Mhe. Jaji Harold Nsekela kuwa Kamishna wa Maadili katika Sekretariat ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Jaji Rehema Kiwanga Mkuye kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Jaji Sivangilwe Sikalaliwa Mwangesi kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi vitendea kazi Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Jaji Jackobs Mwambegele kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com