WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepiga marufuku uchapaji holela wa vitabu vya kufundishia na kujifunzia kwa wachapaji binafsi na badala yake uchapaji huo utasimamiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TEA) ili kuthibiti ubora.
Amesema mbali na kudhibiti wa ubora pia uamuzi huo unalenga kuwa na kitabu kimoja kwa kila somo kwa kila mwanzfunzi kwa nchi nzima ili kuweka uwiano mzuri katika ufundishaji na upimaji wa wanafunzi .
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Desemba 2, 2016) wakati akizungumza na walimu wa halmashauri ya Jiji la Arusha na wilaya ya Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Arusha.
Ziara hiyo inalenga kukagua utelelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,Utendaji wa Serikali, kusikiliza na kujionea kero zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo kwa kushirikiana na viongozi wa Mkoa ili kuweza kuzitafutia suluhisho.
Amesema kipindi cha nyuma vitabu vilikuwa vinachapwa na watu mbalimbali hivyo kusababisha malalamiko makubwa kutokana na vitabu hivyo kuwa na makosa mengi. “Sasa vitabu vikibainika kuwa na makosa tutaibana Taasisi ya Elimu Tanzania,”.
Aidha, amesema Serkali itahakikisha kila mtoto anakuwa na kitabu chake ili kuwawezesha kusoma vizuri na kuwa na uelewa wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuwarahisishia walimu katika ufundishaji.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu madeni ya walimu, ambapo amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutenga fedha katika mapato yao kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi mbalimbali katika maeneo yao wakiwemo walimu.
Awali Waziri Mkuu alizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Jiji na wilaya ya Arusha na kumuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Arusha kumchunguza Ofisa Utumishi wa wilaya ya Arusha, Bi. Imelda Isosi kufuatia tuhuma za rushwa, ufisadi, unyanyasaji kwa watumishi zilizotolewa dhidi yake.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada watumishi hao kupewa fursa ya kumuuliza maswali ambapo mhudumu wa Chumba cha kuhifadhia maiti wa Hospitali ya Ortumet Wilayani Arusha, Bw. Bernard Mtei kudai kwamba halmashauri ya wilaya ya Arusha inanuka ufisadi na rushwa hususan katika sekta ya afya.
Baada ya kutoa madai hayo Bw. Mtei alimkabidhi Waziri Mkuu nyaraka mbalimbali zenye uthibitisho wa madai hayo, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo amuhakikishia Waziri Mkuu kwamba watafanya uchunguzi wa kina dhidi ya tuhuma hizo na zikithibitika wahusika watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria
Wakati huo huo Waziri Mkuu ameitaka Idara ya Uhamiaji kudhibiti wahamiaji haramu kwa kuanza kufanya misako katika nyumba za kulala wageni ili kuwabaini wageni wanaoingia nchini bila ya kibali kwani ni chanzo cha kuingiza silaha haramu nchini.
Amesema inashangaza kuona silaha za aina nyingi katika maeneo mbalimbali ambazo Tanzania hakuna ambazo zinadaiwa kuingia nchini kupitia maeneo ya mpakani. “Hivyo ni lazima Idara ya Uhamiaji ihakikishe wanadhibiti uingiaji wa wahamiaji kwenye mipaka mbalimbali nchini,”.
Waziri Mkuu amesema Serikali haizuii wageni kutoka mataifa mengine kuingia nchini ila ni lazima udhibiti wa wageni hao ufanyike ikiwa ni pamoja na kujiridhisha sababu za kuja nchini na muda watakao kuwepo.
Hata hivyo aliwasihi watumishi wa idara mbalimbali za Serikali kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu, weledi, uadilifu na kuwatumikia wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali hata kama wamekosea kuuliza katika maeneo yao.
Amesema “baadhi ya wananchi hawana uelewa juu ya wapi wapeleke malalamiko yao lakini kwa kuwa wewe ni mtumishi wa umma unapaswa kumsikiliza na kumwelekeza aende wapi badala ya kumtolea maneno yasiyofaa,”.
Social Plugin