Mwenyekiti mpya wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda ametamba kuwa ataimarisha uhusiano wa kisiasa kati ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Rais John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM.
Shibuda ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, alitoa tambo hizo jana, ikiwa ni dakika chache baada ya kuchaguliwa kuongoza baraza hilo kwa kipindi cha miaka miwili katika uchaguzi uliofanyika jijini Dar akichukua nafasi ya Peter Kuga Mziray wa APPTMaendeleo kilichofutwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
Shibuda alisema atatumia fursa, uzoefu na uwezo alionao kuhakikisha vyama vyote vinakuwa na matumaini ya ushiriki wa kisiasa kupitia heshima ya baraza hilo.
“Nimepokea kwa furaha matokeo haya lakini najua nina mzigo mbele yangu. Hilo la mahusiano ninamtanguliza Mungu anisaidie ili kuhakikisha naotesha matumaini mapya katika baraza hili. Nitakunjua vizibo vyote vilivyoziba katika mahusiano haya, ushirikiano wa siasa zetu uwe kwa masilahi ya Watanzania na utaifa wetu,” alisema mbunge huyo wa zamani wa CCM na Chadema.
Shibuda aliibuka mshindi baada ya kupata kura 20 dhidi ya mpinzani wake, Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda aliyefuata kwa kura 14.
Jumla ya kura 36 zilipigwa huku mbili zikiharibika. Katibu wa CCK, Renatus Muabhi alipongeza ushindi wa Shibuda huku akitoa angalizo kuwa asikubali kutumika kulinda masilahi ya kundi la chama kilichopo madarakani.
“Namwamini kwa uzoefu wake atasaidia kurejesha heshima ya baraza hilo ila kama atayumbishwa, sisi tuko tayari kushawishi kura ya kumwondoa madarakani,” alisema.
Wengine waliogombea kiti hicho ni Hashim Rungwe (Chaumma), Anna Mghwira (ACT), Fahmy Dovutwa (UPDP), Hassan Kisavya (NRA), na John Cheyo wa UDP ambaye alijitoa.
Baadhi ya vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi huo ni Sauti ya Umma (Sau), CUF, CCM, DP, Demokrasia Makini, Jahazi Asilia, Ada-Tadea, CCK na Chadema.
Baraza la Vyama vya Siasa ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka jukwaa la kujadiliana masuala yenye masilahi kwa Taifa na uimarishaji wa mfumo wa vyama vingi nchini.