Profesa
Idris Mtulia aliyefariki dunia jana, ameacha pengo katika sekta ya afya
huku wagonjwa zaidi ya 20 wakimsubiri awafanyie upasuaji.
Daktari
wa Hospitali ya Tumaini, Profesa Chalonde Yongolo (aliyewahi kufanya
kazi na Profesa Mtulia) alisema licha ya kuwa mwalimu wake, alikuwa
akishirikiana naye kufanya kazi hospitalini hapo.
Profesa
Mtulia (pichani) aliyefariki dunia ghafla nyumbani kwake Upanga jijini
Dar es Salaam jana asubuhi imeelezwa alikuwa mchapakazi, mwenye maadili
msaada mkubwa kwa jamii.
“Ni
pigo kubwa, leo alikuwa na wagonjwa 20 ambao walitarajia kupata huduma
ya upasuaji. Nimepokea taarifa za msiba huu saa sita mchana na kwa
mujibu wa mke wa marehemu kifo chake ni cha ghafla kwa kuwa aliamka
salama na alipata kifungua kinywa na akaenda kupumzika na kupitiwa na
mauti.”
Profesa Mtulia aliwahi kuwa mbunge wa Rufiji na Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Mkurugenzi
wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema licha ya kuwa alikuwa amemaliza muda
wake lakini Profesa Mtulia aliitumikia bodi hiyo kwa kipindi cha miaka
mitatu.
“Bado alikuwa mshauri katika mambo mbalimbali yahusuyo bodi.”
Bwanakunu alisema Profesa Mtulia alikuwa mchangamfu, mcheshi na huru kuzungumza na watu wote pasipo kujali rika.
“Hakuwa
mtu wa kawaida, alikuwa daktari hivyo alifanya majukumu yake kama mtu
anayeelewa vizuri kitu anachokifanya na hata baada ya kumaliza muda wake
mchango wake ulikuwa ni muhimu.
"Alikuwa mtaalamu wa afya, msikivu na mpenda haki aliyehakikisha watu wanapata huduma kwa muda mwafaka."
Social Plugin