WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Jeshi la Polisi kufanya upelelezi kuwabaini waliohusika na mauaji ya watu saba ambao miili yao iliokotwa pembezoni mwa mto Ruvu wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani, ikiwa kwenye mifuko ya sandarusi, ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kuokotwa kwa miili hiyo Desemba 8, mwaka huu na kueleza kuwa matukio kama hayo, likiwemo la mjasiriamali kuuawa baada ya kutekwa mkoani Tabora, hayavumiliki wala kukubalika.
Alitoa maagizo hayo jana katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililofanyika kitaifa kijijini Shelui wilayani Iramba mkoani Singida. Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Alisema, “Serikali kwa kushirikiana na Polisi, tena Waziri wa Mambo ya Ndani uko hapa (akimzungumzia Mwigulu Nchemba aliyekuwepo katika baraza hilo), tutaendelea na upelelezi ili wahusika wachukuliwe hatua kali.”
Jana akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Star TV, Mwigulu alisema uchunguzi umebaini kuwa miili saba iliyookotwa Bagamoyo ni ya wahamiaji haramu.
Miili ya watu sita ilikutwa Desemba 7, mwaka huu kando ya mto Ruvu wilayani Bagamoyo ndani ya mifuko ya sandarusi na ikiwa imewekwa mawe ili isielee kisha mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni.
Mwili mwingine uliokotwa Desemba 9, eneo hilo hilo na pamoja na kutokuwa katika mfuko wa sarandusi, ulikuwa umevuliwa shati na kuonekana na majeraha mgongoni na kwenye ubavu umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi alisema miili yote ilizikwa kwa kuwa ilikuwa vigumu kuwatambua kutokana na kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho chochote kinachoashiria watu hao ni nani na wametoka wapi na kwamba Polisi inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika na mauaji hayo na atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Waziri Mkuu alisema serikali ipo macho kukabiliana na tishio lolote la usalama na vyombo vya usalama vipo tayari muda na wakati wote.
Aliwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa wanapoona kuna hatari kwani viongozi wa dini na waumini wa dini hizo ndio walinzi wa Taifa.
Alisema uwepo wa vikundi vya uhalifu kama ‘panya road’ cha jijini Dar es Salaam ni hatari kwa jamii, kwani vinadhuru na kuvuruga amani na kueleza kuwa ni vijana na watoto wanaoishi katika jamii, walioko misikitini na makanisani na kutaka waripotiwe katika vyombo vya usalama ili washughulikiwe.
Alizungumzia ugaidi na kubambikizwa kesi, na kusema serikali itaendelea kusimamia mtu kupata haki zake na anayestahili adhabu, kuipata vile vile.
“Ni heri kuwa na watu 10 waliotoroka mahabusu kuliko mtu mmoja kukaa mahabusu kwa kesi ya kuonewa,” alisema Majaliwa.
Mwigulu anena kuhusu miili 7, Saanane
Akizungumza jana kwa simu kuhusu vifo hivyo vya Bagamoyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alisema serikali baada ya tukio hilo ilichukua hatua kupitia vyombo vya usalama na tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amemhakikishia wanalifanyia kazi.
“Kama nilivyosema awali, hatujajua asilimia mia kwa mia kama watu hao waliouawa wana connection (uhusiano) na wahamiaji haramu waliookotwa wamechoka sana hivi karibuni (juzi).
“Kuna wahamiaji 81 waliokotwa hawajitambui, wameishiwa nguvu kabisa, ni eneo hilo hilo kulikookotwa miili hiyo, tumehisi watu waliowabeba wahamiaji hao inawezekana wengine walikufa na kwa vile hawana utu, wakawafunga katika viroba (sarandusi) na kuwatupa, Polisi wanachunguza hili kwa kina,” alieleza Mwigulu.
Aidha, alisema pia Polisi inachunguza ikiwa miili hiyo ilitupwa kikatili na wasafirishaji wa binadamu ambao nao hawana utu.
Alipoulizwa kwa nini wazikwe haraka bila vipimo vya vinasaba, Mwigulu alisema kuwa alizungumza na IGP na kuelezwa kuwa miili hiyo ilikuwa katika hali mbaya sana, lakini pia kuzikwa hakuzuii uchunguzi kufanyika kujua chanzo cha vifo hivyo.
Kuhusu kupotea katika mazingira ya kutatanisha Ofisa wa Ofisi ya Chadema, Makao Makuu Dar es Salaam, Bernard Saanane Novemba 18, mwaka huu, Mwigulu alisema aliona taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii na kwa kuwa alikuwa akimfahamu, alimpigia simu na kubaini simu haipatikani.
“Nilishtuka kuona hizi habari, binafsi ni rafiki yangu wa karibu, nilipoona hizi habari nilimpigia na sikumpata, baada ya kuona simpati nilimpigia Mbowe (Freeman- Mwenyekiti wa Chadema Taifa), lakini simu yake iliita kama vile mtu yupo nje ya nchi,” alifafanua Mwigulu.
Hata hivyo, alisema amemuagiza IGP awaagize polisi kumtafuta Saanane na kuhakikisha ufumbuzi wa kupotea kwake unapatikana na kujulikana alipo.
Juzi, Mwenyekiti wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), Malisa Godlisten akizungumza na waandishi wa habari, aliipa Chadema na taasisi za umma zenye dhamana ya usalama wa raia saa 72 kuanzia jana kuhakikisha Saanane anapatikana na kueleza umma chanzo cha vifo vya watu hao saba ambao miili yao ilikutwa kando ya mto Ruvu, Bagamoyo.