Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAFANYABIASHARA WA MADINI WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KULAWITI NA KUBAKA WATOTO

Wafanyabiashara wawili mashuhuri wa madini katika miji ya Mererani na jiji la Arusha jana walifikishwa mahakamani mjini Moshi kwa wakikabiliwa na makosa ya ulawiti na ubakaji watoto. 


Mmoja wao, Welaufoo Munisi (38) anashtakiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume wa mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), mwenye umri wa miaka 16. 


Mtoto anayedaiwa kufanyiwa kitendo hicho ni mwanafunzi wa shule moja ya sekondari wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, baba yake ni mchungaji katika usharika ambao tunauhifadhi kwa sababu za kimaadili. 


Akimsomea mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa Kilimanjaro, Joachim Tiganga, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tamari Mndeme alidai kuwa Munisi alitenda kosa hilo Novemba 21, 2016. 


Wakili huyo alidai kuwa siku hiyo katika nyumba za wafanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), mshtakiwa alimlawiti kijana huyo mwenye umri wa miaka 16. 

Kabla ya kufikishwa kortini jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo baada ya kumnyeshwa kijana huyo dawa za kulevya. 


Hata hivyo, Munisi alikana mashtaka hayo na kesi hiyo imepangwa kutajwa Desemba 14 mwaka huu baada ya wakili Mndeme kuiambia Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo ulikuwa haujakamilika. 

Dhamana yake ilikuwa wazi na alitakiwa kuwa na wadhamini wawili na hadi saa 8:00 mchana alikuwa hajatimiza masharti hayo.


Wakati Munisi akikabiliwa na shtaka hilo, mfanyabiashara mwingine wa Mererani, Benedict Kimario (42) jana alipandishwa kizimbani mjini Moshi, akikabiliwa na mashtaka ya kumlawiti na kumbaka mtoto wa miaka minane. 

Wakili Mndeme alidai mbele ya Hakimu Mkazi, Idan Mwilapo kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo Mei 10 mwaka huu katika Kijiji cha Mrau, Wilaya ya Rombo, Kilimanjaro.

Mshtakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Joseph Peter, alikana tuhuma hizo na kesi hiyo imepangwa kutajwa kesho ili kuangalia kama ametimiza masharti ya dhamana au la baada ya jana kukwama. 


Alikwama baada ya Hakimu Mwilapo kumtaka kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja angesaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni, lakini wakajitokeza wadhamini ambao si wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro. 


Wadhamini hao walikuwa na barua kutoka Mererani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, ambazo kiutaratibu zilipaswa kwanza kuidhinishwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com