WAKUU wa Wilaya (Ma-DC) na Wakurugenzi nchini, ambao hawajakamilisha kutengeneza madawati, yanayokidhi idadi ya wanafunzi katika shule za maeneo yao, wamepewa siku 14 kukamilisha kazi hiyo.
Imeelezwa kuwa wanafunzi watakapofungua shule, lazima wakae kwenye madawati hayo.
Wakuu wa wilaya na wakurugenzi, watakaoshindwa kutimiza agizo hilo hadi ifikapo Desemba 30, mwaka huu, watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe.
Aidha, wametakiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kwenda kidato kwanza mwakani, wanaanza masomo yao kwa awamu moja, badala ya awamu mbili tofauti.
Agizo hilo lilitolewa jijini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Arumeru katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Aliagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wote nchini kuwa hadi Desemba 30, mwaka huu wilaya zote zenye upungufu wa madawati ziwe zimekamilisha.
“Wale ambao watashindwa kufanya hivyo, watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe” alisema. Akizungumzia ukusanyaji wa mapato katika wilaya hiyo, Majaliwa alisema kuwa hadi Desemba 30, mwaka huu, wawe wamefikia asilimia 50, tofauti na hali ya sasa ambapo wamekusanya asimilia 30 tu. “Ongezeni kasi ya ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zenu na mhakikishe kila mtu anafanya kazi zake kwa kumheshimu mwenzie,” alisema Waziri Mkuu.
Serikali inahitaji haraka madawati ili kuondoa uhaba unaozikabili shule za sekondari na msingi wa madawati. Hali halisi ikoje? Hadi sasa, zaidi ya madawati milioni moja, sawa na asilimia 88 ya madawati yanayohitajika katika shule za msingi na asilimia 95 kwa shule za sekondari, yamepatikana. Kwa shule za msingi, imebaki asilimia asilimia 12 kumaliza tatizo la madawati, huku shule za sekondari imebaki asilimia 5.
Mikoa sita ambayo ina hali mbaya na haijatekeleza kikamilifu agizo hilo la madawati ni Mwanza, Kigoma, Mara, Rukwa, Simiyu, Dodoma na Geita, ambapo Geita inadaiwa madawati zaidi ya 80,000 ya shule za msingi na sekondari.
Mwanza inadaiwa madawati 41, 438, Kigoma madawati 31,171, Mara madawati 16,978, Dodoma madawati 14,873, Rukwa madawati 10,978 pamoja na Mkoa wa Simiyu.
Mkoa wa Mwanza unaundwa na wilaya za Nyamagana, Ilemela, Misungwi, Kwimba, Ukerewe, Magu na Sengerema, wakati wilaya za mkoa wa Kigoma ni Buhigwe, Uvinza, Kakonko, Kasulu, Kibondo na Kigoma.
Wilaya za mkoa wa Mara ni Tarime, Bunda, Butiama, Musoma, Serengeti na Rorya na Mkoa wa Rukwa una wilaya za Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.
Mkoa wa Simiyu wilaya zake ni Bariadi, Maswa, Busega, Meatu, Itilima na Mkoa wa Dodoma wilaya zake ni Kondoa, Bahi, Mpwapwa, Kongwa, Dodoma, Chamwino na Chemba, wakati mkoa wa Geita wilaya zake ni Geita, Chato, Bukombe, Mbogwe na Nyang’hwale.
Mikoa ambayo imemaliza tatizo hilo la madawati kwenye shule za msingi na sekondari ni 14 ambayo ni Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Mbeya, Ruvuma, Njombe, Manyara, Pwani, Shinyanga, Singida na Tabora.
Mikoa mingine iliyosalia, imebakiza idadi ndogo ya madawati ambayo inakaribia kukamilika. Tanzania Bara ina mikoa 26.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin