HALMASHAURI ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga, imewavua madaraka walimu wakuu 15 wa shule za msingi wilayani humo, kwa kosa la kuandikisha wanafunzi hewa 883 na kuisababishia halmashauri hiyo hasara ya Sh milioni 3.4.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege, alisema hatua hiyo imetekelezwa baada ya kufanya uchunguzi wa kuhakiki wa wanafunzi hao kwa kipindi cha kuanzia Agosti hadi Oktoba mwaka jana katika shule za msingi.
Berege alisema katika uhakiki wa kwanza uliofanyika Agosti hadi Oktoba, mwaka jana, ilibainika kuwepo kwa wanafunzi hewa 639.
Aliongeza kuwa katika uhakiki mwingine uliofanyika Oktoba mwaka huo kwa kushirikiana Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) walibainika wanafunzi hewa 244.
Alisema kutokana na tatizo hilo, halmashauri hiyo iliwaita walimu hao wakuu na kuwataka warudishe fedha hizo na walikubali kuzirudisha fedha katika Ofisi ya Mkurugenzi kabla ya kuvuliwa madaraka yao rasmi kuanzia Desemba 7, mwaka huu walipokabidhiwa barua zao.
Mkurugenzi huyo aliwataja waliovuliwa madaraka na shule kwenye mabano kuwa ni Emmanuel Nkwabi (Mhama) aliyelipa Sh 56,000 Sita Kasangi (Mwakuzuka) aliyelipa Sh 132,000, Iman Gongo (Nyamigege) amelipa Sh 155,000, Fabian Mchiwa (Mwanyaguli) Sh 21,000 na Omari Masani (Ngaya) Sh 86,000.
Aliwataja wengine kuwa ni Vedastus Masonga (Buganzo) Sh 215,5000, Bernard Patroba (Nyamididi) Sh 142,000, Abbas Kirua (Gulla) aliyelipa Sh 26,000, Elisafi Mshana (Shishinulu) Sh 456,500, George Mabambi (Mbizi) Sh 68,000 na Hussen Said (Bukwangu) Sh 56,000.
Wengine ni Anthonia Peter (Chella) Sh 168,000, Godfrey Niwagira (Buyange) Sh 99,000, Aron Sizya (Kashishi) Sh 198,400 pamoja na Jovinus Katemi (Nyakadoni) aliyelipa Sh 99,000.
Kwa upande wake, Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Msalala, Vivian Masangya, alisema walimu wakuu wa shule za msingi katika halmashauri yake wanatakiwa kuhakikisha kila mwezi wanatoa taarifa za wanafunzi.
Aidha, aliwataka wawe makini katika kutoa takwimu mbalimbali za wanafunzi.
Masangya aliongeza kuwa sasa Serikali inataka kuona watumishi wake wakiwemo walimu wanafanya kazi kwa kufuata miongozo pamoja na weledi na kuongeza kuwa kwa sasa serikali hapendi kuona fedha zake zinapotea kirahisi kama ilivyokuwa kwa walivyofanya walimu hao.
IMEANDIKWA NA RAYMOND MIHAYO,-habarileo KAHAMA
Social Plugin