HALMASHAURI ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, imeanza msako wa kuwatembelea walengwa wanaonufaika na Mfuko wa Jamii (TASAF) Awamu ya Tatu.
Zaidi ya watu 80 wamekamatwa na kufikishwa mahabusu ya Kituo cha Polisi Bariadi kwa kudaiwa kufisadi fedha hizo.
Akizungumzia hilo mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Abdallah Malela alisema kuwa jumla ya kaya 80 katika halmashauri hiyo, zinatafutwa ili zirejeshe fedha zote.
Alisema imebainika kuwa kaya 80 ziliingizwa katika mradi wa TASAF III kwa njia za kinyemela na kuchukua Sh milioni 17.8.
“Ni kweli kuna msako huo, jumla ya kaya 80 hazikustahili kuwemo katika mpango huu, tulifanya ukaguzi mpya baada ya maelekezo kutoka Serikali Kuu kututaka kupitia upya walengwa, kama wanakidhi vigezo vya kuwemo kwenye mpango,” alieleza Malela. Alisema kaya hizo zilibainika kutokuwa na vigezo.
Ziliandikiwa barua tangu Agosti mwaka huu, kutaka warejeshe fedha zote za miezi sita zilizotolewa kwao. Alieleza kuwa baada ya kupatiwa barua hizo, hakuna kaya hata moja ambayo imeanza kurejesha fedha hizo.
Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa msako huo wa nguvu. Alisisitiza kuwa wahusika hawatapewa dhamana mpaka warejeshe fedha zote.
“ Watu ambao tumewakamata hawapewi dhamana mpaka warejeshe fedha za serikali. Mpaka leo tumefanikiwa kurejeshewa kiasi cha Shilingi milioni 1.1 kati ya milioni 17.8,” alieleza Malela.
Alisema msako huo utaendelea kwa halmashauri nzima mpaka pesa zote zirejeshwe, ili kuweza kutumika kwa walengwa ambao walikusudiwa katika mpango huo.
“ Leo ni siku ya tatu tunahangaika kupata dhamana, mama yetu amekamatwa, wamesema ili kupata dhamana mpaka arejeshe kiasi chote ambacho amepokea. Tangu aanze kuchukua fedha za TASAF anadaiwa shilingi 240,000,” alisema mmoja wa mtoto wa mnufaika, ambaye hakutaka kutaja majina yake.
Mwenyekiti wa mtaa ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema kuwa wao kama viongozi wa mtaa waliletewa barua kutoka TASAF wilaya, yenye majina ya watu ambao walikuwa kwenye mpango huo na wanatakiwa kurejesha fedha zote kutokana na kutokidhi vigezo.
“ Nilipokea barua ikiwa na majina ya watu wanaotakiwa kurejesha fedha zote walizochukua toka waanze kupokea, wanasema wao hawakustahili kuwemo katika mpango huo, wengi wanadaiwa zaidi ya shilingi 200,000” alisema Mwenyekiti huyo.