Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANANCHI WAUA MTUHUMIWA ALIYETOROKA POLISI


MTUHUMIWA wa uhalifu sugu kutumia silaha za jadi, unyang’anyi na mauaji, aliyetoroka chini ya ulinzi wa Polisi mwanzoni mwa wiki, Shukuru Jokeri (25) mkazi wa kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro, ameuawa na wananchi baada ya kumkuta akiwa mtaani.

Wananchi walimkuta juzi Desemba 13 na kisha kumshambuliwa vikali na baadaye kufariki dunia akipatiwa matibabu hospitalini baada ya polisi kumnasua mikononi mwa wananchi waliokuwa wakimpiga.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na alisema alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na wananchi wa mtaa wa Chamwino, kata ya Chamwino, Manispaa ya Morogoro, Desemba 13, mwaka huu saa 4 :45 usiku.

Kamanda Matei alisema baada ya kugundua kwamba ndiye aliyetoroka Polisi walimkamata na kumshambulia.

Alisema mtuhumiwa huyo Desemba 8, mwaka huu, alikamatwa kwa kosa la mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha aina ya panga na kufikishwa Polisi na alipokuwa anaendelea kuhojiwa, Desemba 12, mwaka huu alitoroka.

Hata hivyo, alisema Desemba 13, mwaka huu mtuhumiwa huyo alionekana uraiani ambapo wananchi walipomwona waliamua kumkamata na kumshambulia.
Via>>Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com