WANAWAKE wanne katika Kijiji cha Kihumbu, Kata ya Hunyari wilayani Bunda, wamejeruhiwa kwa kupigwa na vitu vizito, zikiwamo fimbo, rungu, bapa za panga na katani, baada ya kutuhumiwa kumuua kwa uchawi, mwanafunzi Waryo Mseti (12).
Tukio hilo lilitokea juzi mchana katika kijiji hicho wakati mwili wa mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Kihumbu ukisubiri kuzikwa.
Ilidaiwa kuwa baada ya Mseti kufariki dunia, wazazi wake kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hasha Hamisi, walikwenda kupiga ramli kwa mganga wa kienyeji wakidai mtoto huyo alikufa kifo cha ushirikina.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Chacha Warioba, alidai mganga huyo baada ya kufanya dawa zake, alieleza kuwa mwanafunzi huyo alikuwa amechukuliwa kichawi na wanawake hao na alikuwa bado yuko hai ila walikuwa wamemficha sehemu.
“Nathibitisha ni kweli tukio hilo lipo, polisi walifika hapa kijijini na kuwachukuwa wanawake hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Bunda. Wakati tukio hilo linatokea mimi sikuwapo hapa kijijini,” alisema Warioba.
Inadaiwa kuwa Hamisi aliyewapeleka wazazi wa mwanafunzi huyo kwa mganga, aliwaeleza wenzake kuwa hata yeye aliwaona wachawi hao kwenye kioo cha maji ya mganga wa jadi.
Kauli hiyo ilithibitishwa kwa waombolezaji waliokuwapo nyumbani hapo wakati maiti ya mtoto huyo ikiwa ndani ikisubiri kuzikwa.
Baada ya kuelezwa hayo, baadhi ya waombolezaji walianza kuwasaka wanawake hao wanaotuhumiwa kwa uchawi.
Waliwakamata mmoja baada ya mwingine na kuwapeleka mlimani, huku wakiwa wamewafunga kamba na wakiwatishia kuwachinja. Waliwapiga na kuwataka wamrudishe mtoto huyo.
Wanawake hao (majina tunayo), wote wakazi wa Kijiji cha Kihumbu, walisema walifanyiwa unyama na ukatili huo unaohusisha imani za ushirikina, na hata nyumba ya mmoja wao ilimwagiwa mafuta iweze kuteketezwa kwa moto.
“Walitupiga sana kwa fimbo, mabapa ya mapanga, rungu na katani, walituteka hadi milimani wakitulazimisha tumrudishe huyo mtoto waliodai tumemuua.
“Mimi walinilaza chini na wakaniwekea panga shingoni, eti wanichinje kama sitaki kusema ukweli. Lakini nilikataa kwamba sijui chochote,” alisema mmoja wa wanawake hao.
Wanawake hao waliokolewa na polisi waliofika katika eneo la tukio na kuwachukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi Bunda kabla yakuwapeleka katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda (DDH).
Bado wamelazwa hospitalini hapo baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo na muuguzi wa zamu katika Wodi ya Wanawake, Daria John, alisema hali zao zinaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhani Ng’anzi, alisema wote waliohusika kujichukulia sheria mkononi lazima wakamatwe na kufikishwa mahakamani.