Watoto watatu wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 12 wamekufa maji baada ya kuzama katika bwawa lililopo eneo la Ziwamboga, Mombasa wilaya ya Magharibi B, mjini Unguja.
Taarifa ya vifo hivyo imetolewa na daktari wa uchunguzi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Msafiri Marijani.
Daktari huyo alisema watoto hao walikufa baada ya kukosa hewa ya oksijeni baada ya kuzama katika bwawa hilo.
Miili ya watoto hao wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 12 ilifikishwa katika hospitali kuu wa Mnazi Mmoja mjini Unguja majira ya saa sita na nusu mchana.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi kutoka mkoa wa Mjini Magharibi, watoto waliokufa ni Ahmed Mjaka Kombo, Fessal Abrazak Mjaka na Mundhir Sheha Khamis wote wakazi wa Ziwamboga, Mombasa Mjini Unguja.
Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema watoto hao walifika katika bwawa hilo kwa lengo la kuogelea ambapo wawili walizidiwa maji na kuanza kuzama ambapo yule wa tatu aliwafuata wenziwe kwa lengo la kuwaokoa na yeye kuzama.
Imeelezwa kuwa ni kawaida ya watoto kuogolea kwenye bwawa hilo, japo huzuiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B, Silima Haji amewataka wananchi kuacha shughuli za uchimbaji mchanga katika maeneo yasiyo rasmi ili kuepusha matukio yanayozuilika huku diwani wa wadi ya Mombasa akitoa mwito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa kuwazuia watoto wao kucheza katika madimbwi ya maji.