WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu Bi. Theresia
Mahongo kuhakikisha mashine zote za kupampu maji zilizoko ndani ya mita
500 kutoka kwenye chanzo cha maji cha Qangded ziwe zimeondolewa ifikapo
saa 12.00 jioni ya jana na atakayekaidi atachukuliwe hatua za kisheria.
Alisema
kitendo cha kuweka mashine za kupampu maji karibu na chanzo hicho na
kuvuta maji kwenda kwenye mashamba yao kinasababisha maji kushindwa
kufika katika mashamba ya wakulima wengine hivyo amewataka wafuate
utaratibu uliowekwa na waendeshaji wa mradi huo.
Waziri
Mkuu alitoa agizo jana Jumatatu, Desemba 5, 2016 wakati akizungumza na
wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Jobaji
kata ya Baray wilayani Karatu, ambapo alisema Serikali haitavumilia
kuona mtu mmoja akivuruga mradi huo wa umwagiliaji.
Alisema
ili kuhakikisha mradi huo wa umwagiliaji unakuwa endelevu lazima chanzo
cha maji kilindwe na wananchi wasiruhusiwe kufanya shughuli za kijamii
karibu na chanzo na badala yake wasogee umbali wa mita 500.
“Sitaki
kuona mashine zikipampu maji ndani ya mita 500 kutoka kwenye chanzo na
badala yake wakulima wote wafuate taratibu zilizowekwa . Lazima chanzo
kilindwe kwa sababu maji yakikauka mazao nayo yatakauka, hivyo tutakosa
chakula jambo ambalo hatutaki litokee. Mkuu wa wilaya kesho nenda
kafanye ukaguzi katika chanzo ukikuta mashine kamata,” alisema.
Awali,
Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji safi na salama wa kijiji cha Jobaj
unaotekelezwa na shirika la World Vision Tanzania uliogharimu sh.
milioni 285. Mradi huo utahudumia vijiji vitatu vya Kata ya Baray
ambavyo ni Mbunga Nyekundu, Jobaj na Dumbechand.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Miradi wa Wolrld Vision Tanzania, Bw.
Revocutus Kamara alisema mradi huo unatokana na hitaji kubwa la maji
katika vijiji hivyo vitatu na uwepo wa kisima kirefu cha maji
kilichochimbwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mwaka 2009.
“Mradi
huu wa maji unatekelezwa kwa awamu tatu, awamu ya kwanza ilianza Machi
hadi Novemba 2016, ambapo wakazi 5,272 ikiwa ni pamoja na taasisi nne za
Serikali ambazo ni Zahanati, Magereza, shule ya msingi na sekondari
zilizoko katika kijiji cha Jobaj wananufaika kwa kupata maji safi na
salama,” alisema.
Alisema awamu ya pili na ya tatu ya mradi huo itaanza Disemba 2016 na itagharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Akizungumza
kuhusu mradi wa umwagiliaji Mkurugenzi huyo alisema shirika lao
limechangia kuboresha miundombinu ya umwagiliaji kwa kujenga kilomita
1.716 za mfereji katika kijiji cha Jobaj (kilomita moja) na Dumbechand
(mita 716) ambapo umegharimu zaidi ya sh. milioni 210 na inalenga
kunufaisha zaidi ya wakulima 4,450 wa vijiji hivyo.
Alisema
mifereji hiyo itawezesha wakulima katika vijiji hivyo kuwa uhakika wa
upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya
chakula na biashara hivyo itasaidia kupunguza migogoro ya maji, kuongeza
eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 803 hadi hekta 1,203.