Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mzee Yusufu Makamba asema Rais Magufuli anafanana na Yohana Mbatizaji kwa vile ni kiongozi anayefanyakazi bila kuogopa.
Makamba ametoa kauli hiyo leo kwa njia ya simu katika mahojiano maalum na Mwandishi wa habari hizi. Alisema kuwa Rais ni kiongozi mchapakazi ambaye hayumbushwi na maneno wala vitisho kwa vile anasema ukweli katika kutekeleza majukumu yake.
“Yohana Mbatizaji alisema ukweli na hakutikiswa na upepo, hakuogopa macho ya watu wala hakuwa mtu wa majigambo, kama ilivyoandikwa katika Biblia Takatifu Marko 6:12, na hivyo ndiyo navyomfananisha Rais wetu Magufuli na viongozi wote tumuunge mkono” alisema Makamba.
Aidha, kuhusu miaka 55 ya Uhuru , alisema kuwa ni vyema Watanzania wakazingatia wito wa uhuru ni kazi, na kwa kuwa Serikali hii imeweka mkazo katika ufanyaji kazi.
Makamba alisema kuwa katika Awamu hii ya HAPAKAZI TU, inaakisi wito wa Uhuru katika vipindi mbalimbali kuanzia kipindi cha Uhuru ni kazi na Uhuru na kazi mara baada ya kupatikana kwa Uhuru na kuwakumbusha watanzania kuulinda Uhuru.
“Ni lazima kuulinda Uhuru kwa gharama yeyote ili amani na mshikamano uendelee kuwepo basi hatuna budii kuepuka lugha zenye maneno ya uchochezi, ukabila na udini” alisema Makamba