NB-Picha haihusiani na habari hapa chini |
MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Bahati Mbula (43) mkazi wa Kanindo Kata ya Kishiri amefariki dunia kwenye mkesha wa mwaka mpya baada ya kudaiwa kunywa pombe za kienyeji kupita kiasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema hilo ni tukio pekee lililotokea katika mkesha wa mwaka mpya mkoani Mwanza.
“Nimepata taarifa moja tu ya mtu mmoja kufariki huko Kanindo, marehemu huyo anadaiwa kunywa kwa kuchanganya pombe za aina nyingi za kienyeji.
“Nimeambiwa marehemu huyo alitoka eneo la Sawa Kata ya Lwahnima na kwenda kunywa huko Kanindo, sasa usiku huo wenzake walidhani ameondoka kurudi kwao kumbe alikuwa ameanguka njiani karibu na pale alipokuwa akinywa pombe hiyo,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema Jeshi la Polisi linafuatilia kwa uchunguzi zaidi kama alikuwa anaumwa au kuna kitu kingine.
“Tuliwaambia wananchi washerekee mwaka mpya bila kuleta madhara yoyote ikiwamo kuchoma moto matairi, kuendesha magari ovyo, kurusha mawe nadhani watu walizingatia ndiyo maana hata matukio ya uhalifu hayakuwapo,” alisema.
NA SHEILA KATIKULA-MWANZA
Social Plugin